Habari

Ijumaa, 14 Februari 2014

Ngombale - Mwiru kateuliwa ujumbe wa bunge la katiba akiwakilisha waganga wa kienyeji.

                                           Mh.Ngombale Mwiru



SIRI ya uteuzi wa mkongwe wa siasa nchini, Kingunge Ngomale-Mwiru, kuingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba imefichuka.

Habari ambazo gazeti hili limezipata, zilisema kuwa uteuzi wa mkongwe huyo wa siasa nchini umepitia katika Chama cha Watabibu wa Tiba Asili nchini (ATME).

Habari kutoka ndani ya chama hicho, zinasema kuwa wao wenyewe kwa matakwa yao walilipendekeza jina la mwanasiasa huyo wakiamini kwamba atawazungumzia mambo yanayowahusu ndani ya Bunge hilo linalotarajiwa kuanza Februari 18 mjini Dodoma.

Kwa mujibu wa Mratibu wa ATME taifa, Boniventura Mwalongo, chama cha waganga wa kienyeji kilipendekeza jina la Kingunge na kwa bahati nzuri ameteuliwa.

Alisema kuwa watu wanapaswa kufahamu kuwa Kingunge ni mlezi wa chama hicho tangu mwaka 1999 na hii imetokana na yeye kuwa mstari wa mbele kutetea tiba hiyo ambayo inapigwa vita na wamiliki wa hospitali.

Mwalongo alisema mwanasiasa huyu hata kipindi cha kwanza cha uongozi wa Rais Jakaya Kikwete alipoteuliwa kuwa mbunge, alihakikisha hoja za tiba asili zilipokuwa zikipenyezwa bungeni alikuwa mstari wa mbele kuziongelea tofauti na wabunge wengine.

Alisema walianza kufanya kazi na Kingunge tangu kipindi cha uongozi wa Rais Benjamin Mkapa, alipokuwa Wizara ya Serikali za Mitaa na mara nyingi walikuwa wakikutana naye kwenye mikutano yao kila walipomhitaji.

“Nakumbuka neno alilokuwa akipenda kulitumia ni kwamba sasa nakwenda kuzungumza na ‘wachawi’, akiwa anamaanisha sisi, na kipindi hicho watu walikuwa bado hawajajua thamani yao.

“Sasa kupitia chombo chako mwandishi naomba uueleweshe umma wa Watanzania kwamba Kingunge hajapendelewa na rais kama watu wanavyodhani, bali yeye ni mmoja wa watu walioteuliwa katika makundi maalumu kama rais alivyoagiza awali, hivyo wamuache mzee wa watu akafanye kazi,” alisema mtabibu huyo.

Mwenyekiti wa ATME, Simba Abrahaman Simba, alisema uteuzi wa Kingunge ulifanywa kwa kufuata katiba ya chama chao katika mkutano walioitisha baada ya Rais Kikwete kukaribisha orodha ya majina ya watu kutoka asasi za kiraia na taasisi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Simba, hata wakati wa kikao cha kumteua na kupeleka jina lake kwa Rais Kikwete, Kingunge mwenyewe hakuwepo, hivyo walimpigia simu kumuomba akubali pendekezo la chama hicho kumtaka awe mjunge kupitia kundi lao, jambo ambalo aliliafiki.

Alitaja majina mengine yaliyokuwa katika orodha ya watu waliowapeleka mbali na Kingunge kuwa ni Othman Shem, Richard Chinzepo, Sara Mwakibete, Zahra Mandemla, Heldgade Kiwasira na Baeatrice Madeyane.

Kama vile haitoshi, mwenyekiti huyo alisema hata siku majina ya wajumbe wa Bunge la Katiba yalipotangazwa, Kingunge  hakuwa na taarifa hadi walipompigia simu kumfahamisha kwamba rais amemteua.
Juzi katika mkutano wake na waandishi wa habari, Jukwaa la Katiba Tanzania lilihoji uteuzi huo wa Kingunge, kupitia kundi la asasi za kiraia wakati hajawahi kuwa mwanachama wa asasi yoyote.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Jukwaa la Katiba, Hebroan Mwakagenda, alisema nafasi 20 walizokuwa wametengewa asasi za kiraia, majina matano ni ya wanasiasa na makada wa CCM.

Alitolea mfano kwa Kingunge, akisema ameingizwa kwenye kundi la asasi wakati hajawahi kuwa na asasi wala hawajawahi kumshuhudia hata kwenye msiba wa mwanaharakati mwenzao.

“Watuambie Kingunge wamemtoa wapi na asasi yake ilisajiliwa wapi na inaitwaje… mimi nimekuwa kwenye asasi kwa miaka 22, lakini sijawahi kumwona hata kwenye msiba wa mwanaharakati mwenzetu, sasa iweje leo hii aibukie kwenye kundi la asasi?” alihoji Mwakagenda.

Kingunge anena
Akizungumza kuhusiana na hilo, wakati alipokuwa akiagwa jana na watabibu hao, Kingunge alisema tangu awali alivyopigiwa simu na ATME alisita kukubali moja kwa moja akijua lazima kuna watu watasema sana kuhusu uteuzi wake.

Hata hivyo aliongeza kwamba baada ya kufikiria sana akaona kama atakataa waliomteua wasingejisikia vizuri na ndiyo maana aliamua kukubali ombi lao.

Kingunge alisema kelele za uteuzi wake katika mambo mbalimbali ya taifa ameshazizoea na kudai kwamba wanaomsema ni wale wanaojua moto wake pindi anapoamua kusimamia na kulitetea jambo flani.

Bunge la Katiba 
Kuhusu Bunge la Katiba, mwanasiasa huyo alisema wajumbe wote watakaoingia wanatakiwa kwenda kutunga katiba bora na si katiba mpya kama inavyosemwa.

“Unajua kama ni katiba tayari tunayo siku nyingi, kinachotakiwa ni kuboresha yale mazuri yaliyopo, kuondoa upungufu na kuibua mambo mapya ambayo yatakuwa na faida kwa wananchi,” alisema.

Pia alitumia fursa hiyo kuwaonya wanasiasa au watu wanaodhani katiba inaenda kutungwa kwa ajili ya kuwatengenezea mazingira ya kuendelea kuwa madarakani au kwa wale wasio madarakani kuingia Ikulu.
“Hapa lazima wabunge walioteuliwa watulize kichwa kwelikweli, sio kwenda kusaidia kundi flani kwenda Ikulu au kuendelea kuwa madarakani, kwani mimi pamoja na kuwa CCM, siendi kuwaandikia wao katiba kwani inatakiwa iwe ya matabaka yote,” alisisitiza.

Tiba asili
Kingunge alisema Watanzania bado wamekuwa na dhana potofu kuhusu tiba mbadala na wengine kuifananisha na ushirikina.

Akitolea mfano alisema kwa nchi za Korea, Asia na India zote hizo zilipitiwa na wakoloni, lakini jambo la kwanza walipojikomboa kulishughulikia lilikuwa ni tiba za asili.

Alisema nchi hizo zimekuwa zikitumia tiba inayotokana na mimea na madini yanayopatikana nchini mwao, vitu ambavyo hata Tanzania tunavyo, lakini watu wamekuwa wakividharau.

Pia alisema ieleweke kwamba afya ya wananchi ni suala muhimu na la kwanza, hivyo ushiriki wa ATME umetambuliwa katika katiba kama njia mojawapo ya kuweka misingi ya utoaji tiba nchini.

Chanzo:TANZANIA DAIMA FEB 15,2014

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni