Habari

Jumatano, 2 Oktoba 2013

Mabadiliko yanakuja, salama ni kuyapokea


Salim Said Salim
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeelezea kwa masikitiko makubwa juu ya kile ilichokiona kuwa ni mwamko mdogo wa watu kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Kauli hii ya ZEC inatokana na watu wachache kujitokeza kufanya hivyo katika mchakato uliomalizika hivi karibuni wa kuwaandikisha wapiga kura wapya katika daftari hilo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti mpya wa ZEC, Jecha Salum Jecha, waliojitokeza ni watu 30,999, sawa na asilimia 22.7 tu kati ya 136,697, waliokisiwa.
Kauli ya ZEC inashangaza na kukwepa ukweli. Hali hii ni kielelezo cha watu kukosa imani na namna ambavyo chaguzi zimekuwa zikiendeshwa Zanzibar.
Kwanza ni wazi kwamba kupiga kura Zanzibar bado sio haki ya raia, bali ni kama kupewa zawadi na ZEC inayoamua nani apewe haki hiyo na nani anyimwe.
Kwa maana nyingine kuwa Mzanzibari na kuwa na sifa za kuandikishwa kupiga kura haitoshelezi kupewa haki ya kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Hadi sasa uamuzi wa nani apige kura ni wa sheha ambaye huangalia zaidi kama huyo anayetaka kujiandikisha ni ‘mwenzetu au sio mwenzetu’.
Uhuni ambao baadhi ya hawa masheha wameufanya katika chaguzi zilizopita unaweza kuandikiwa kitabu cha kuchekesha na kusikitisha. Hii inatokana na baadhi yao kuwanyima haki ya kupiga kura watoto, ndugu na majirani zao.
Bila aibu hawa masheha wamedai kutowajua watu hawa, wakiwemo wale ambao ni baba zao. Lakini kwa vile huo ni mpango maalumu hapana hata sheha mmoja aiyefunguliwa mashitaka ya kusema uongo na kutenda kosa la jinai la kumnyima raia haki ya kupiga kura.
Mara nyingi tumesikia kwamba kipengele cha kutaka mtu kuwa mkazi wa eneo kwa muda wa miaka mitatu (zamani miaka mitano) katika eneo moja kimesababisha maelfu ya watu kunyimwa haki ya kupiga kura.
Hapa nataka kwa mara nyingine kuweka wazi kwamba kama sheria za Zanzibar ni za kidemokrasia na zenye utawala bora, basi huyo mtu angalau apewe haki ya kupiga kura kwa uchaguzi wa rais.
Hii ni kwa sababu visiwa vya Unguja na Pemba ni jimbo moja kwa uchaguzi wa rais wa Zanzibar na eneo lolote lile la Tanzania ni jimbo moja la uchaguzi wa rais wa Muungano. Kwa hivyo mtu awe anaishi popote pale (hata baharini au juu ya mti), madhali ni Mzanzibari basi awe na haki ya kuchagua rais wa Zanzibar na wa Muungano.
Lakini watu hawa wamekuwa watazamaji tu wa chaguzi na wapo waliotishiwa kufunguliwa mashitaka kwa sababu tu wametaka kujiandikisha kupiga kura.
Usiri juu ya namna kura zilivyopigwa bado una shaka, maana wapo waliofukuzwa kazi serikalini kwa sababu hawakupigia kura chama cha CCM. Hata Rais mstaafu, Komandoo Salmin Amour, bila ya aibu alisema wazi kuwa hakuona sababu ya kuwapa kazi serikalini watu ambao hawakumpigia kura.
Waziri wa zamani wa Elimu wa Zanzibar, Omar Ramadhani Mapuri, hawezi kusahaulika kwa kuwafukuza shule zaidi ya wanafunzi 100 wenye asili ya Pemba waliotaka haki yao ya kujiandikisha kupiga kura kwa vile walitimiza umri wa miaka 18. Hadi hii leo Mapuri hajawaomba radhi vijana wale na Wazanzibari kwa uamuzi wake ule uliokwenda kinyume na sheria na kuathiri maisha yao na familia zao.
Mapuri anapokumbushwa uchafu huu huruka na kuwataka watu wasitoneshe vidonda wakati yeye ndiye aliyevisababisha.
Kama Tume ya Uchaguzi ilikuwa inafanya shughuli zake kwa uwazi basi ingekuwa na ubavu wa kusema watu wangapi walinyimwa kujiandikisha katika zoezi hilo. Hii itatoa sura ya jinsi hali ya uandikishaji ilivyo hivi sasa.
Unapowauliza Wazanzibari wengi  juu ya mtizamo wao kwa ZEC jawabu unalopata kutoka kwao ni kwamba hiyo ni tume ya kuwachuja wapiga kura na sio kuwapa watu haki ya kupiga kura. Hii ni kusema watu wengi bado hawana imani na namna ZEC inavyoendesha shughuli zake.
Kwa miaka nenda rudi masheha wamekuwa kikwazo kikubwa katika kuifanya demokrasia ichanue na kustawi Zanzibar na licha ya mapendekezo kadhaa ya kuwadhibiti watu hawa serikali inajifanya haisikii na ndio kwanza inawaongezea madaraka.
Ukichunguza sifa za watu hawa kuchaguliwa kuwa masheha, utagundua manyago mengi. Miongoni mwao ni misimamo yao ya kisiasa sio taaluma na uwezo kazi.
Wapo walioamua kuwatendea haki raia na kukataa kujiingiza katika kapu la kuonea na kudhulumu watu. Matokeo yake ni kufukuzwa kazi, kuadhiriwa na kuakashifiwa kwa vile wameonekana “sio wenzetu”.
Kwa tafsiri ya wakubwa waliopo madarakani “wenzetu” ni watu ambao wanawanyima wenzao haki ikiwa pamoja na ile ya kupiga kura.
Jingine ambalo lina dosari katika utoaji haki Zanzibar ni utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari. Idara ya Vitambulisho imefanya marekebisho makubwa kutaka kuhakikisha kila mwenye haki ya kupata kitambulisho anapewa haki hiyo na imekuwa haina vikwazo kusikiliza malalamiko ya wananchi.
Lakini hao masheha hawasikii la muadhini wala mteka maji msikitini. Wapo ambao badala ya kujenga mashirikiano na wananchi katika sehemu zao wamejijengea uhasama usiokuwa na faida.
Njia pekee itayovutia watu kuwa na imani na ZEC na kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kupiga kura ni kuhakikisha kwamba kura sio zawadi, bali ni haki ya kila Mzanzibari.
Siku hizi watu waliopo nje ya nchi zao wanayo haki ya kupiga kura, lakini kwa Zanzibar hata mtu ambaye hajawahi kuvuka bahari na kwenda nje ya visiwa vya Unguja na Pemba hana haki hiyo.
Huu ndio ukweli na wapo wanaonuna ukiwekwa hadharani. Kama hawataki maovu wanayoyafanya yaelezwe hadhari basi wasiyatende.
Vile vile wale wote, hasa masheha na akina fulani (wenyewe wanawajua) wanaowanyima watu haki yao ya kupiga kura katika chaguzi za nchi yao wachukuliwe hatua za kisheria.
Kumnyima mtu haki ya kupiga kura ni kosa kubwa la uvunjaji wa haki za binadamu, na kama kweli tunaheshimu basi sheria za kuwadhibiti na kuwatia adabu wanaozivunja zionekane zinachukuliwa.
Tuache porojo za kujigamba kwamba tuna utawala bora na wa kidemokrasi wakati tunacheza ngoma ya kudanganyana.
Tuwe wakweli au tutajikuta historia inatuumbua na kutuhukumu siku za mbele kwa maovu tunayoyatenda hii leo. Tujifunze haraka na tena kwa uadilifu kwa tunayoyaona na kuyasikia  yanayowakuta wengine katika nchi za nje ambao walitumia vibaya madaraka yao kuonea wananchi wengine.
Waswahili wanasema ‘mambo kangaja…huenda yakaja’ na wakitaka wasitake hayo mabadiliko yanakuja na njia pekee ya salama ni kuyapokea, tena kwa heshima na adabu na sio kwa shingo upande na nongwa.
Zama za kuonea watu kwa wapi wanatoka, udhaifu wao au misimamo yao ya kisiasa zimepitwa na wakati na hazirudi. Kwa ufupi zama hizo zimeshakwenda arijojo.
Ni vizuri sote tukabadilika kabla ya wakati haujatulazimisha kubadilika na hatimaye kuona aibu kwa tunayoyatenda hivi sasa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni