Habari

Jumatano, 2 Oktoba 2013

Sheikh Ponda akwaa kisiki


2nd October 2013
Chapa
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda
Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Morogoro, imetupilia mbali ombi liliwasilishwa na upande wa utetezi wa kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh   Ponda Issa Ponda, la kuitaka kumfutia shtaka la kwanza au kulihamishia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam ikisema zote zina mamlaka sawa kisheria.

Ombi hilo liliwasilishwa na wakili wake, Juma Nasoro Septemba 17, mwaka huu baada ya  mshtakiwa huyo kufikishwa mahakamani hapo kwa mara ya tatu.

Wakili Nasoro aliomba mahakama hiyo kuondoa shtaka hilo la kutotii amri halali linalomkabili mteja wake au lifutwe akidai kuwa ilitolewa na Mahakama ya Kisutu.

Alidai amewasilisha ombi hilo baada kubaini kuwa mahakama hiyo ya Morogoro haina uwezo kisheria kusikiliza shtaka hilo, vinginevyo lifunguliwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambayo ilitoa hukumu hiyo.

Wakili Nasoro ambaye anaongoza jopo la mawakili wawili kumtetea Sheikh Ponda, aliwasilisha ombi hilo baada mahakama hiyo kumnyima dhamana mteja wake kufuatia kupitia vifungu vya kisheria na kukubaliana na ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) lililowasilishwa Agosti 28, mwaka huu kupitia wakili wa Serikali la kufunga dhamana kwa Sheikh Ponda.

Akitoa maamuzi hayo jana, hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Richard Kabate, alisema kwa mujibu wa vifungu mbalimbali vya sheria vya uendeshaji wa kesi za jinai, shtaka hilo dhidi ya Ponda kudaiwa kutokutii amri halali ya mahakama litaendelea kusikilizwa katika mahakama hiyo na siyo kuhamishiwa Kisutu.

Alizitaja sababu za shtaka hilo kuendelea kusikilizwa katika mahakama hiyo kuwa ni mshtakiwa huyo kutenda kosa hilo eneo la Kiwanja cha Ndege la Manispaa ya Morogoro.
Hakimu huyo alisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuhamishiwa shtaka hilo katika Mahakama ya Kisutu hizo zina uwezo wa kisheria kulisikiliza.

Sababu nyingine ni mshtakiwa huyo kuvunja amri halali iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu na siyo sharti kama ambavyo upande wa utetezi ulidai.

Alifafanua kuwa hata kama mahakama hiyo ilitoa sharti, kisheria sharti linalotolewa na mahakama yoyote ni amri.

Kuhusu hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu dhidi ya Sheikh Ponda, alisema ni moja ya vitu ambavyo haviwezi na havina ulazima wa kuthibitishwa kwa kuwa ilitolewa katika mahakama yenye uwezo na uhalali wa kusikiliza.

Katika kesi hiyo jana tofauti na kila ilipotajwa, mawakili wote watatu  wanaomtetea Sheikh Ponda hawakufika mahakamani hapo, hivyo kutetewa na wakili mwingine, Yahaya Njama.

Wakili Njama aliiiambia Mahakama hiyo kuwa, Wakili kiongozi wa utetezi kesi hiyo, Juma Nasoro hajafika mahakamani hapo kwa kuwa yuko nchini India kwa matibabu ya macho.

Alisema Wakili Nasoro atakuwa nchini humo kwa matibabu kwa wiki tatu na kuiomba mahakama hiyo kusogeza mbele kesi hiyo hadi atakaporejea.

Alidai kuwa aliombwa na wakili Nasoro kwenda mahakamani hapo kusimamia kesi hiyo hiyo kutokana na kuwa nje ya nchi kwa matibabu.

Kuhusu mawakili wengine, Bathoromeo Tarimo na Ignas Punge kutofika mahakamani hapo, alidai hana taarifa zozote.

Kitendo cha wakili Njama kutofahamu taarifa za mawakili hao wengine, kilizua mvutano kati yake na upande wa mashtaka.

Mvutano huo ulikuja kwa sababu Wakili Tarimo wakati akimtetea Sheikh Ponda kwa mara ya mwisho aliunga mkono ombi la Wakili Nasoro la kufuta au kuhamishia shtaka la kwanza katika Mahakama ya Kisutu.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Kabate alilazimika kusoma barua iliyoandikwa na Wakili Tarimo ya kutoa udhuru wa kutokuwepo mahakamani jana ikieleza  alikuwa na shughuli nyingine Mahakama Kuu.
Hakimu alihairisha kesi hiyo hadi Novemba 7, itakapoanza kusikilizwa.

Siku hiyo upande wa mashtaka utawasilisha mashahidi 15 na vielelezo vitatu ambavyo ni DVD mbili, hati ya hukumu iliyotolewa Mahakama ya Kisutu dhidi ya Ponda na kibali cha kongamano kilichotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Morogoro.

Sheikh Ponda anayekabiliwa na mashitaka ya kutotii amri halali ya mahakama, kushawishi kutenda kosa na kuumiza imani za dini.

Jana alifikishwa mahakamani saa 4 asubuhi kwa basi la Magereza huku akisindikizwa na magari mengine matano yaliyokuwa yamebaba askari polisi wenye silaha za moto, mabomu ya machozi, virungu, vifaa vya upekuzi na vifaa vingine vya kiusalama.

Watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa Ponda, walikuwa nje ya uzio wa mahakama hiyo wakisema takbir.
Kama ilivyo siku zote wakati wa kesi hiyo ikitajwa,  barabara zinazokatisha mahakamani hapo zilifungwa kwa muda na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, ofisi ya Madini na Hazina Ndogo kwa muda kutokana na ulinzi kuimarishwa.

Baada ya kuharishwa kwa kesi hiyo, wafuasi wa Ponda, walionekana wakiufuata msafara wa magari yaliyokuwa yakimrudisha Ponda kwenye gereza la Segerea huku wakipaza sauti za kumtukuza Mungu kama ishara ya kumsindikiza.

Hii ni mara ya nne kwa Sheikh Ponda  kufikishwa mahakamani hapo.
Kwa mara tatu mfululizo amefikishwa mahakamani hapo kwa  basi hilo la Magereza kutoka Segerea akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi na magereza.

Kwa mara ya kwanza Agosti 19, mwaka huu, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa helikopta ya Polisi na  kurudishwa mahabusu Segerea.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni