Habari

Jumanne, 8 Oktoba 2013

Mkuu wa ulinzi mgodini adaiwa kunyanyasa wananchi

NA MWANDISHI WETU

8th October 2013
Chapa
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga
Wakazi wa Mwadui mkoani Shinyanga wanaoishi ndani ya mgodi wa Williamson uliopo wilayani Kishapu, wamemlalamikia mkuu wa kitengo cha ulinzi wa mgodi huo, David Donda, kuwa anawanyanyasa na kuwafukuza katika eneo hilo kwa njia za uonevu bila kufuata taratibu.

Wamelalamika kuwa, kutokana na hali hiyo, wananchi wenye watoto wanaosoma katika shule ya msingi iliyopo ndani ya mgodi huo wazazi wao wanapofukuzwa kwa amri ya mkuu huyo wa ulinzi wa mgodi huathirika kwa kulazimika kukatisha masomo yao na hivyo kukosa haki ya kupata elimu.

Kwa mujibu wa malalamiko ya wananchi hao waliyoyatuma kwa vyombo vya habari, utaratibu uliowekwa katika mgodi huo, mtu yeyote akitaka kuishi ndani ya mgodi ni lazima apewe kibali cha kuishi katika eneo hilo na kuonyesha muda atakaokaa kibali ambacho kinatolewa na mkuu wa ulinzi wa mgodi huo.

“Tunamuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aingilie kati atunusuru na unyanyasaji tunaofanyiwa ndani ya nchi yetu, tumekuwa kama wakimbizi,” walisema wananchi hao katika taarifa hiyo.

Mkuu wa Ulinzi wa mgodi huo, David Donda alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na tuhuma hizo, alishindwa kuthibitisha wala kukataa badala yake alimtaka mwandishi wa habari kwenda mgodini ili kupata maelezo ya suala hilo badala ya kuzungumza kwa njia ya simu.

 “Wewe njoo mgodi wa Williamson utapata maelezo kama madai hayo ya wananchi ni ya kweli au ya uongo, utakutana na msemaji wa mgodi atayatolea ufafanuzi,” alisema Donda na kukata simu ghafla.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga alipoulizwa, alisema ofisi yake bado haijapata taarifa za kunyanyaswa wananchi hao na kuahidi kutuma vyombo vyake vya usalama kwenda kuchunguza suala hilo ili hatua zichukuliwe.

“Juzi juzi nilikuwa huko Mwadui, inawezekana hili suala wananchi wamekaa nalo wanakataa kueleza viongozi wa serikali, inawezekana hata mkuu wa wilaya halifahamu hili,” alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Wilson Nkambaku, akizungumza na NIPASHE kwa simu alisema yupo Arusha hospitali na kuahidi kulitolea ufafanuzi suala hilo siku yeyote wiki hii.

Wananchi hao katika malalamiko yao, walisema katika kipindi kifupi cha mwaka huu wakazi 23 wametimuliwa eneo hilo kwa kupewa saa 24 na  mkuu huyo wa ulinzi na hivyo kupata wakati mgumu na familia zao.

 Walisema Mkuu huyo wa ulinzi, amepewa dhamana ya kusaini vibali vya wakazi wa Mwadui na anaweza kumfukuza mfanyakazi ndani ya saa 24 katika mgodi huo bila kuulizwa na kiongozi yeyote wa serikali au wa mgodi huo.

Waliongeza kuwa waliokumbwa na adha hiyo wapo ambao wameishi mgodini hapo na kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 wakiwa wameajiriwa katika mgodi huo lakini wanapostaafu kazi na kuajiriwa katika kampuni binafsi ndipo hujikuta wakipewa saa 24 kuondoka mgodini.

Wananchi hao wameliomba Jeshi la Polisi, asasi za kutetea haki za binadamu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuchunguza suala hilo na kwamba wapo tayari kutoa ushirikiano pindi uchunguzi huo utakapoanza kufanywa na vyombo vya serikali.

Afisa Uhusiano wa mgodi huo, Ignas Balyoruguru, alipoulizwa malalamiko ya wananchi hao alisema anaweza akawa anayajua au hayajui na kusisitiza kuwa jambo la msingi ni kwamba mgodi huo una utaratibu wake kwasababu ni eneo linalolindwa.

Alisema mtu anayetaka kuishi ndani ya mgodi huo ni lazima atambulike uhalali wake na akikiuka utaratibu uliowekwa anafukuzwa.

“Mgodi huu ni mgodi uliozuiliwa kama ilivyo migodi mingine, unapoingia kuna utaratibu wake na mtu akifukuzwa kama ana watoto anapewa muda wa kuondoka,” alisema.
Balyoruguru alisema utaratibu wa kuwa na kibali cha kuishi huo umewekwa kwasababu wapo baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu ambao wanafanya eneo hilo kama la kufanyia udanganyifu na ndiyo maana wenye tabia hiyo wakijulikana ni lazima wachukuliwe hatua,” alisema.

Hata hivyo, alisema kama kuna wananchi ambao wamefukuzwa ndani ya mgodi na wanaona hawakutendewa haki wanaweza kupeleka malalamiko yao kwa viongozi wa serikali kama vile Katibu tarafa na siyo kukimbilia kwenye vyombo vya habari.
 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni