JESHI la Polisi nchini lilimshikilia kwa muda kisha kumwachia mwanamke mmoja anayesadikiwa kuwa ni Samantha Lewthwaite ‘Mjane Mweupe’ ambaye amehusishwa katika shambulio la kigaidi lililotokea katika jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi wiki iliyopita.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP), Suleiman Kova, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kulitaka gazeti hili kuwasiliana na msemaji wa jeshi hilo Makao Makuu, Advera Senso.
Kamanda Kova alisema baada ya kufanya uchunguzi waligundua mwanamke huyo si mhusika wa matukio hayo ya ugaidi bali ni mke wa mtu anayeishi hapa jijini.
Akizungumzia tukio hilo, Senso alisema anashukuru mwamko uliopo kwa wananchi ambao walitoa taarifa juu ya kuonekana kwa mwanamke huyo na baada ya polisi kufuatilia walibaini kuwa si mlengwa wa tukio hilo.
“Hapa hakuna stori, ni mwamko walionao wananchi na walifikisha kwa jeshi hili nasi tulifuatilia na baada ya uchunguzi tulibaini hakuwa mhusika…kama unavyopewa taarifa za nyumba fulani kuwa wanauza bangi, lakini ukienda na kufanya upekuzi hakuna hicho kitu, basi tunakuwa tumejiridhisha, ndivyo ilivyokuwa katika suala hilo,” alisema.
Mwanamke huyo alisadikiwa kuwa ni mtuhumiwa wa ugaidi baada ya kwenda katika Benki ya Exim na kutaka kufungua akaunti pamoja na kuomba zabuni ya kufanya usafi katika jengo la benki hiyo lililopo jirani na Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Mmoja wa mameneja wa benki hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini alikiri kuwapo kwa tukio hilo, ingawa hakuwa tayari kutoa taarifa za ndani, kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi wakati tukio hilo likitokea.
Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo, waliozungumza na Tanzania Daima walisema mwanamke huyo alifika katika benki hiyo juzi akiomba zabuni ya kufanya usafi kupitia kampuni yake inayojulikana kwa jina la Osson Breeze.
Walisema hata hivyo baadhi ya watendaji wa benki hiyo waliingiwa shaka na mwanamke huyo kutokana na kufanana na mtuhumiwa huyo wa ugaidi na kutoa taarifa polisi.
Chanzo-Tanzania Daima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni