Habari

Alhamisi, 3 Oktoba 2013

PBZ Bingwa Kuwawezesha Wajasiriamali Tanzania.

Wakurugenzi wakifuatilia maswali ya waandishi wa habari wakati wa kutambulishi ushindi wao.
Mwandishi wa habari akiuliza swali kuhusiana na maendeleo ya kuboresha huduma za PBZ kwa wateja wake na mafanikio ya zoezi lake la kutowa mikopo kwa Wananchi.

                        Wakurugenzi wa PBZ wakifuatilia maswali ya waandishi na kuweka kumbukumbu yao

Msaidizi Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Ame Haji Makame akiinua Kombe la Ushindi Juu kuwaonesha Wafanyakazi wa PBZ kabla ya kumkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ Juma Amour wakati wa sherehe za kusherehekea ushindi huo uliofanyika katika Makao Makuu ya PBZ Islamic Bank Mpirani jengo la Bima.
PBZ Bingwa Kuwawezesha Wajasiriamali Tanzania.


BENKI ya Watu wa Zanzibar (PBZ), imeibuka mshindi wa kwanza kwa kutoa huduma bora na kuwawezesha wajasiriamali nchini Tanzania, katika maonesho ya wiki ya huduma za kibenki yaliyofanyika Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari jana,Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Juma Amour Mohammed, alisema ushindi huo ni ithibati tosha kwamba huduma za benki hiyo zinakubalika.

Mshindi wa pili ni mfuko wa PSPF na nafasi ya tatu imechukuliwa na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.

Maonesho hayo yaliyofanyika Septemba 26-28 yalizishirikisha taasisi za fedha na huduma zinazosaidia maendeleo ya wajasiriamali nchini.

Aidha alisema PBZ itaendelea kutoa huduma bora na kuwawezesha wajasiriamali na kuongeza idadi ya matawi katika mikoa mbali mbali ya Tanzania.

Kuhusu usalama wa benki hiyo, Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa PBZ ni benki salama na kuwahimiza wafanyabiashara na wananchi kuendelea kuweka fedha zao.

Alisema PBZ ina uwezo wa kuhimili mtikisiko wa kifedha unapotokea, inatoa huduma za uhakika na ina mtaji unaokidhi vigezo vya BoT.

Kuhusu uwakala wa benki, alisema benki hiyo itaanzisha wakala wa benki (banking agency) hasa vijijini ili kuongeza idadi ya wananchi wanaofaidika na huduma za kibenki popote walipo.

Mfumo huo ambao unatumiwa na baadhi ya benki, umeongeza wingi wa wananchi wanaotumia huduma za kibenki hasa katika maeneo ya vijijini ambako benki nyingi hazijafungua matawi yake.

“Ujenzi wa matawi ya benki ni gharama kubwa, lakini mfumo huu utaongeza idadi ya wananchi wanaofaidika na huduma za kibenki lakini pia ni nafuu kuuanzisha,” alisema.

Alisema tayari BPZ imeshaomba kibali BoT ambayo ndio msimamizi kuanzisha huduma hiyo.

Aidha alisema benki hiyo imeanza kutoa mikopo ya nyumba inayowalenga wateja wakubwa, wa kati na wadogo ambayo ukomo wake wa kulipa ni hadi miaka 15.

Alihimiza wateja wa benki hiyo kuchangamkia fursa hiyo ili kupata makaazi bora na salama.

Akizungumzia maendeleo ya matawi mawili ya PBZ yaliyopo Dar es Salaam, alisema yanafanya vizuri na kwa pamoja yana akiba inayozidi shilingi bilioni 40.

Kuhusu wizi unaofanywa katika mashine za ATM, Mkurugenzi huyo alisema benki imejipanga kukabiliana na wizi kwa kuweka kifaa maalum kuzuia wizi huo.

“Tutaweka ‘anti skimming devices’ ili kuzuia wezi kunyonya alama za siri za mteja anapokwenda kuchukua fedha kwa ATM,” alisema.

Katika maonesho hayo yaliyofunguliwa na Waziri, Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Mhe. Mary Michael Nagu mshindi wa kwanza alikabidhiwa kombe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni