Ijumaa, 04 Oktoba 2013 12:31
Polisi ya Kenya imetangaza kuwa, watu wanne akiwemo Sheikh Ibrahim Ismail Rogo wameuawa baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana ndani ya gari dogo jana usiku huko mjini Mombasa.
Taarifa ya Polisi ya Kenya imeeleza, Sheikh Ibrahim Rogo alikuwa mrithi wa Sheikh Aboud Rogo ambaye naye aliuawa na familia yake kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwezi Agosti 2012.
Mauaji ya Sheikh Ibrahim Rogo ambayo yameutikisa mji wa Mombasa, yametokea baada ya kupita takriban wiki mbili tokea kundi la al Shabab lilipovamia na kuua watu wasiopungua 63 na kujeruhi mamia ya wengine kwenye jengo la maduka ya biashara la Westgate jijini Nairobi.
Baadhi ya wananchi wa Mombasa wanakituhumu kikosi maalumu cha kupambana na ugaidi kuwa ndicho kilichotekeleza mauaji hayo. Sheikh Ibrahim Rogo ambaye alikuwa akitoa mihadhara kwenye Msikiti wa Musa mjini Mombasa alituhumiwa na jeshi la polisi kuwa anawachochea vijana wa Kiislamu kujitumbukiza kwenye makundi ya kigaidi.
Polisi ya Kenya imesema kuwa, Gaddafi Mohammad, Issa Abdallah na Omar Abu Rumeisa ni miongoni mwa waliouawa, naye Salim Aboud alinusurika kwenye shambulio hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni