Habari

Alhamisi, 24 Aprili 2014

Wabunge wamporomoshea matusi

Mwenyekiti  wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ameendelea kushambuliwa kwa lugha kali, matusi na kejeli yeye binafsi na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na Tume yake kupendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu.

Safari hii Jaji Warioba ameshambuliwa kwa maneno makali na Hawa Ghasia, kwa kumueleza kwamba, afunge mdomo’ wake na kukaa kimya kwa kuwa kazi yake ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba imekwisha.

Ghasia ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), alitoa kauli hiyo juzi usiku alipokuwa akichangia mjadala wa rasimu ya katiba sura ya kwanza na ya sita, ambazo pamoja na mambo mengine, zinazungumzia jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wa Muungano.


Akizungumza kwa hisia kali, Ghasia alisema Jaji Warioba anatakiwa kuacha kuzungumzia na kutetea mapendekezo ya Tume, kwani kufanya hivyo kunaashiria kuwa rasimu ya katiba iliyowasilishwa kwa wajumbe na Tume, siyo maoni ya Watanzania, bali yake (Jaji Warioba).

Alisema kazi ya Jaji Warioba na Tume yake ilikuwa ni kukusanya maoni, kuyachambua na kuyapeleka kwenye Bunge hilo, lakini baada ya hapo ameendelea kuwa mpigia debe muundo wa serikali tatu.

“Napenda kuungana na Mheshimiwa Mjumbe, ambaye alisimama hapa akasema baada ya Jaji Warioba kutuletea rasimu na kuiweka mezani na hotuba aliyotoa zaidi ya masaa manne, kazi yake imeisha, sasa afunge mdomo, akae kimya, aliachie Bunge hili lifanye kazi na baada ya hapo tutaenda kwa wananchi,” alisema Waziri Ghasia.

Aliongeza: “Kadri anavyoendelea kupiga kelele, Mheshimiwa Jaji Warioba sasa anatutia wasiwasi kwamba, yale siyo maoni ya wananchi, bali ni maoni yake. Ndiyo maana anayatetea.”

“Kama ni maoni ya wananchi, sisi ndiyo wawakilishi wa wananchi, tuachwe tuseme, lakini sisi siyo mwisho. Tutakwenda kwa wananchi na wenyewe wataamua kukubaliana na yale tuliyoyajadili au kukataa.”

Waziri Ghasia alisema Tume ya Jaji Warioba ilikuwa na wajumbe 30, lakini wenzake wote wamekaa kimya ila yeye (Warioba) kila siku kwenye vyombo vya habari anasikika akizungumza kwamba, serikali tatu haziepukiki.

“Kwani yeye (Jaji Warioba) kazi yake ilikuwa ni kupiga debe au kukusanya maoni ya wananchi?” alihoji Ghasia.

Ghasia alisema Jaji Warioba kuendelea kusema kuhusu rasimu ya katiba, inaonyesha kuwa alikuwa na kazi mbili, ya kukusanya maoni ya wananchi na kuhoji kwa nini maoni ya mabaraza ya katiba ya wilaya, hayakuchukuliwa na kuingizwa katika rasimu hiyo.

“Kati ya mabaraza 784, ni manne tu yalichukuliwa, hata ukichambua yale mengine kuona walichosema hawakufanya, hivyo kwa kuwa hayakuendana na maoni yao. Napenda kusema sisi ndio tunatunga Katiba na changamoto za Muungano si suluhisho la kuanzisha serikali nyingine,” alisema Ghasia.
 
BULEMBO
Abdallah Bulembo akichangia mjadala huo jana, alimshambulia Jaji Warioba na kumtuhumu kuwa hana nia njema kwa Watanzania walio wengi.

Bulembo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, alisema: “Sisi tuna nia njema, Mzee Warioba anataka kuangamiza nchi hii kwa matakwa yake.”

Alisema yeye alikuwa mtu wa kwanza kumsema Jaji Warioba na kwamba, baada ya kumsema mwaka jana akiwa ziarani mkoani Tanga, watu wengi walimshambulia.
“Nilipomsema kuwa hana nia njema mwaka jana nikiwa Tanga, kuna watu walinipigia simu wakisema sina adabu,” alisema.

Alidai kuwa Jaji Warioba siyo mwadilifu kwani mwaka 1991 alipata kutoa rushwa ya nyama kwenye uchaguzi na akapoteza uwaziri na ubunge pia kuzuiwa kugombea kwa miaka mitano.

Ingawa Bulembo alimtaja Warioba kwa tuhuma hizo, kiongozi ambaye alipotea ubunge kwa amri ya mahakama ni Stephen Wasira katika jimbo la Bunda na pia kuzuia kugombea kwa miaka mitano kwa sababu ya rushwa. Wasira alichauana na Warioba katika uchaguzi wa Bunda mwaka 1995 Wasira akipeperusha bendera ya NCCR-Mageuzi.

KOMBA AWAVAA WARIOBA, BUTIKU, SALIM
Mjumbe mwingine, John Komba, aliwashambulia Jaji Warioba na wajumbe wawili wa tume hiyo, Joseph Butiku na Dk. Salim Ahmed Salim, kwamba walikuwa watu wa karibu sana na Mwalimu Julius Nyerere, lakini leo wamemsaliti na wanataka kuua Muungano kwa kusema kuwa Mwalimu angekuwa hai angetaka muundo wa Muungano ubadilishwe.

Komba ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), alisema asingewataja wajumbe wengine wa tume zaidi ya Jaji Warioba, Butiku na Dk. Salim kwa kuwa walikuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere, huku akisema kuwa walikuwa wanakunywa naye chai na mkate na hata wakati mwingine ukitaka kumuona ni lazima uwaone wao kwanza.

“Hawa walikuwa karibu naye. Usingeweza kumuona bila wao, ndugu hao walikunywa naye chai na mkate, lakini leo hii ndiyo wanaotaka kuuvunja Muungano,” alisema Komba, ambaye alikuwa anatumia neno ‘Warioba and Company’ kila wakati.

“Endapo Bunge hili halitapitisha muundo wa Muungano wa serikali mbili na kupitisha wa serikali tatu, nitaingia msituni kudai muundo wa serikali mbili,” alisema Komba.

Dk. Titus Kamani, ambaye ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, hakulitaja moja kwa moja jina la Jaji Warioba, lakini alisema:
“Viongozi wa kitaifa wasiukubali ushauri wa watu wasio na nia njema na nchi yetu.”

Tangu kutoka kwa rasimu ya katiba, watu kadhaa wengi wakiwa ni viongozi na makada wa CCM, wamekuwa wakimshambulia na kumkosoa Jaji Warioba binafsi badala ya kujadili maudhui ya Rasimu ya Katiba.

Imeandikwa na Jacqueline Massano, Theodatus Muchunguzi na Abdallah Bawazir (Dodoma).
 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni