Habari

Jumatano, 15 Oktoba 2014

MSF: WHO, AU zinazembea katika vita dhidi ya Ebola


Mkuu wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka nchini Afrika Kusini ameukosoa vikali utendaji dhaifu na mbovu wa Shirika la Afya Duniani WHO na Umoja wa Afrika AU katika kampeni za kukabiliana na usambaaji wa kasi wa maradhi ya Ebola magharibi mwa Afrika. 
Sharon Ekambaram ameeleza hali ya kusikitisha inayolikabili eneo la magharibi mwa Afrika na kusisitiza kwamba, Shirika la Afya Duniani na Umoja wa Afrika zimekuwa zikitoa ahadi tu na kuelezea tishio la ugonjwa huo kwenye vyombo vya habari. 

Ekambaram ameelezea shughuli za timu ya madaktari wasio na mipaka katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita huko magharibi mwa Afrika kwa lengo la kuzuia kusambaa maradhi ya homa ya Ebola na kusisitiza kwamba, wafanyakazi wa shirika hilo wamepata ushirikiano mdogo kutoka jamii ya kimataifa.

Mkuu wa Shirika la MSF nchini Afrika Kusini amesema kuwa, Shirika WHO huko Geneva na Zurich limekuwa likijuhusisha tu na utoaji wa takwimu za watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo. 

Sharon Ekambaram ameongeza kuwa, hivi sasa balozi nyingi za kigeni zimefunga ofisi zao katika nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea na kwamba misaada ya jamii ya kimataifa, WHO na AU kwa wahanga na familia za wahanga wa Ebola imekuwa michache mno. 

Inafaa kuashiria hapa kuwa, zaidi ya watu 8,000 wameshaambukizwa maradhi ya Ebola, na zaidi ya 4,000 wameshafariki dunia.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni