Habari

Jumapili, 9 Novemba 2014

KUHUSU RAIS KIKWETE KUZUIA KAMPENI YA KATIBA MPYA, IKULU YATOA KAULI NZITO.


Ikulu imesema kuwa Rais Jakaya Kikwete hajazuia kufanyika kwa kampeni kuhusu Kura ya Maoni isipokuwa Sheria ya Kura ya Maoni ndiyo inayozuia  kufanyika kwa kampeni hizo kwa sasa.
 
Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Salvatory Rweyemamu alisema hayo Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa sheria hiyo inaelekeza kampeni kufanywa ndani ya siku 60 kabla ya kufanyika ya kupiga kura ya maoni.
 
“Kimsingi Rais hajakataza kampeni, Sheria ya Kura ya Maoni ndiyo inayokataza, lakini kinachofanyika ni kutoa elimu kama inavyofanya Serikali, hiyo inaruhusiwa...Serikali haifanyi kampeni, nasisitiza,” alisema.
 
Rweyemamu alisema hayo baada ya Rais Kikwete kuwahutubia Wazee wa Mkoa wa Dodoma, Jumapili iliyopita.
 
Alipoulizwa kuwa Ikulu inafanya kazi ya asasi za kiraia zilizoainishwa kwa mujibu wa sheria kufanya kampeni za kuelimisha umma kuhusu Kura ya Maoni, Rweyemamu  alisema Ikulu inatoa somo la uraia lakini si kupiga kampeni.
 
Alipotakiwa kueleza kama ni elimu, kwanini inawataka Watanzania kupiga kura ya ndiyo, Rweyemamu alisema:

“Tunatoa civic education (elimu ya uraia) na hiyo ya  kusema wapige kura ya ndiyo, haikatazwi kwani wapi kuna sheria inayokataza Serikali kutoa elimu?”
 
Hata hivyo, Rweyemamu alisema kuwa Serikali ndiyo yenye mchakato wa Katiba hivyo haikatazwi kupigia kampeni.
 
“Utakaaje kimya wakati watu wanapiga kampeni huko? Sisi tumeingia mtaani baada ya wengine kufanya hivyo, japokuwa kuna utaratibu wake,” alisema.
 
Kauli ya JK Dodoma
“Ninaomba Watanzania wenzangu tuzingatie mamlaka ya Sheria ya Kura ya Maoni ambayo imeelekeza vizuri lini kura ya maoni itapigwa na lini kampeni zitafanyika na lini wadau watatoa elimu, naomba tuwe na subira. Tukizingatia sheria hii hakuna  ugomvi,”alisema Rais Kikwete.
 
Alisema ni vyema kusubiri hadi tume itakapotoa maelekezo ya utekelezaji huo kwa kuwa muda wa kampeni na utoaji elimu kwa umma bado.
 
Rais Kikwete alisema sheria ipo na imepangwa siku maalumu za kufanya hivyo.
 
Alisema licha ya sheria kuruhusu kampeni kufanyika ndani ya siku 60 kabla ya kura za maoni kupigwa, kwa mamlaka yake ya kiungozi, kura na kampeni vitafanyika ndani ya siku 30 tu.
 
“Kampeni zitaanza Machi 30 na kumalizika Aprili 29 ikiwa ni siku moja kabla ya kupiga kura ya maoni. Muda huo ndiyo utakuwa wa kufanya hivyo,” alisema Rais Kikwete.
 
Kuhusu Waraka
Akizungumzia waraka ulionaswa na Ukawa, Rweyemamu alisema wamesema waraka ni wa siri, lakini si wa siri, ni mapendekezo ya kuitangaza katiba kupitia vyombo vya habari.
 
Alisema Ukawa wanazungumzia mpango wa Serikali kutumia fedha za umma kwa ajili ya kufanya kampeni, lakini Ukawa wanatumia fedha nyingi mikoani kufanya kampeni ya kuikataa Katiba.
 
Katika mkutano wao na waandishi wa habari, viongozi wa Ukawa walieleza kunasa waraka wa mkakati unaofanywa na Ikulu kutaka kuidhinisha fedha za umma Sh2.5 bilioni kwa ajili malipo kwa vyombo vya habari vitakavyotumika kushawishi  wananchi kuipigia kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa.
 
Akizungumzia hilo Rweyemamu alisema kilichofanyika ni kupeleka dokezo kwa Katibu wa Rais akitaka kuidhinishiwa fedha hizo ili kampeni za kushawishi wananchi zianze kupitia vyombo vya habari.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni