Makamu Wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddialisema kasi ya uwekezaji nchini inaweza kuongezeka mara dufu iwapo wananchi watazingatia zaidi uimarishaji wa mazingira hasa katika mtandao wa mawasiliano.
Alisema wawekezaji wengi huvutika na hali ya mazingira safi yanayowashawishi kupanua wigo wa mtandao huo ambao husaidia kupatikana kwa huduma zote za msingi za mawasiliano kwa upande wa simu, posta na utangazaji.
Balozi Seif alieleza hayo wakati akizindua mtambo maalum wa usimamizi wa masafa ya mawasiliano Zanzibar hafla iliyofanyika katika Ofisi ya Mamlaka ya mawasiliano Tanzania { TCRA } iliyopo Chukwani nje kidogo ya Maji wa Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha mfuko wa mawasiliano kwa wote ili kuunga mkono juhudi za wawekezaji binafsi na washirika wa maendeleo katika ujenzi wa miundo mbinu ya mawasiliano kwenye maeneo ya vijijini ambayo kibiashara bado hayajavutia wawekezaji.
Alieleza kwamba Serikali imefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 na Dira ya Taifa ya Tanzania ya mwaka 2015.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza wawekezaji ambao uamuzi wao wa kuwekeza hapa nchini hususan kwa visiwa vya Unguja na Pemba umesaidia kukua kwa sekta ya mawasiliano na kuboresha njia za mawasiliano Visiwani.
Balozi Seif alisema ujio wa wawekezaji hao umesaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa gharama za mawasiliano ya simu na utangazaji ikiwa ni pamoja na kuongeza pato la Taifa.
Ametoa wito kwa wawekezaji zaidi kutumia fursa iliyopo nchini hususan mazingira mazuri ya kisiasa na udhibiti bora wa kuwekeza kwenye ujenzi wa miundo mbinu ya mawasiliano hapa Nchini.
Akizungumzia utekelezaji wa uamuzi wa shiria la umoja wa Mataifa la mawasiliano ya simu { ITU } wa kubadilisha teknolojia ya utangazaji wa Televisheni kutoka analogi kwenda Digitali uliofikiwa na mwaka 2006 hadi 2015 Balozi Seif alisemaq Taasisi zinazohusika lazima zihakikishe watumiaji wa huduma hizo hawaathiriki.
Balozi Seif alizikumbhusha Taasisi hizo kufanya ukaguzi maalum wa kitaalamu kwenye maabara na kuidhinisha viwango vyake kwa ving’amuzi vinavyoingizwa hapa Nchini.
Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na juhudi za kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi kwa ving’amuzi na Televisheni za Digitali ili wananchi wenye kipato cha kawaida wamudu kuvinunua.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameishukuru mamlaka ya mawasiliano kwa kufikia uamuzi wa kuweka mtambo maalum wa kusimamia masafa ya mawasiliano Zanzibar.
Alisema hatua hiyo ni busara ambayo itaiwezesha Zanzibar kudhibiti matmizi mazuri ya masafa pamoja na huduma za mawasiliano kwa wananchi.
“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefarajika kwa kutimiza wajibu wenu na kuhakikisha kuwa Zanzibar pia inakuwa na uwezo wa kusimamia masafa muda wote bila ya kusubiri mtandao kama huo kutoka Tanzania Bara “. Alisisitiza Balozi Seif.
“ Nafurahi kuona Tanzania hivi sasa inajipanga kwenda kisasa zaidi “. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akitoa Taarifa fupi ya mtambo wa usimamizi wa masafa ya mawasiliano hapa Zanzibar Mkurugenzi Mkuu bwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } Profesa John Nkoma alisema maslahi ya watumiaji wa mawasiliano nchini yanapaswa kulindwa wakati wote.
Profesa Nkomo alisema Masafa ndio rasilmali katika Nyanja za mawasiliano hivyo juhudi za kuendeshwa kitaalamu ni la msingi hasa ikizingatiwa ushindani mkubwa uliopo hivi sasa wa sekta ya mawasiliano miongoni mwa makampuni tofauti ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi mkuu huyo wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania aliihakikisha Jamii kwamba mtambo huo utakuwa ukitoa huduma kwa ufanisi na kuboresha mawasiliano kwa wananchi walio wengi Nchini.
Mapema Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri yua Muungano wa Tanzania Profesa Makame Mnyaa Mbarawa alisema Wizara hiyo iko mbioni kutunga sheria mbali mbali ili kuleta ufanisi zaidi katika upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano.
Profesa Mbarawa alisema hatua hiyo imekuja kufuatia sekta ya mawasiliano duniani kuendelea kukua na kubadilika kwa haraka kiteknolojia.
Alieleza kuwa ukuaji wa kisekta umepelekea kuundwa kwa mamlaka ya mawasiliano kwa lengo la kuratibu mawasiliano ndani ya jamuhuri ya Muungano wa Tanzania isipokuwa Sekta ya utangazaji kwa Upande wa Zanzibar kwa vile tayari ina Tume yake ya Utangazaji.
Profesa Mbarawa alifahamisha kwamba Mtambo huo maalum wa usimamizi wa masafa ya mawasiliano Zanzibar uliogharimu shilingi Milioni mia saba na hamsini za Kitanzania { 750,000,000/- } utasaidia kuviweka salama vyombo vya usafiri Angani na Baharini Nchini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/9/2013.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni