Habari

Jumatatu, 23 Septemba 2013

SMZ YAANGALIA UWEZEKANO WA KULIFANYIA MATENGENEZO ENEO LA UWANJA VIWANJA VYA MICHEZO LA MNAZI MMOJA.

 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaangalia utaratibu muwafaka itakaochukuwa wa kuona  jinsi gani inaweza kulifanyia matengenezo makubwa eneo zima la uwanja wa Michezo la Mnazi Mmoja ili lirejee katika uhalisia wake wa kuhudumia kundi kubwa la wanamichezo ndani ya Manispaa ya Mji wa Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiyafunga rasmi mashindano ya soka ya Kombe la Dr. Sheni ya Jimbo la Kiembe Samaki kwenye mchezo wa Fainali uliozikutanisha Timu za soka za Small Ziko iliyoibuka bingwa kwa kuifunga  Timu ya sokaya  Hibron kwa  Goli 1-0.
Bao hilo pekee la ushindi la Timu ya Soka ya Small Ziko liliwekwa kimiani na wingi machachari wa timu hiyo Yunus  Mariano Albano katika Dakika ya 40 ya kipindi cha pili baada ya heka heka  kubwa iliyotokea langoni mwa Timu ya Hibron.
Balozi Seif ambae alishuhudia pambano hilo la kuvutia la fainal ya Dr. Sheni Cup  hasa katika kipindi cha pili cha mchezo huo alisema eneo la uwanja wa michezo la Mnazi Mmoja hivi sasa liko katika hali mbaya inayosikitisha kiasi cha nusu ya eneo hilo kushindwa kutumika kimichezo.
Alisema tatizo kubwa linalosababisha  kuharibika kwa uwanja huo hivi sasa  ambalo linastahiki kufanyiwa utafiti na utaalamu mkubwa ni kile kitendo cha kuingia kwa maji ya bahari ambacho hakikuwepo kipindi cha nyuma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali imejikita zaidi katika kuona michezo tofauti iliyofifia hapa Zanzibar  inafufuka tena kwa kuimarisha pamoja na kuhuisha viwanja vya michezo ili kufikia lengo hilo.
Aliwapongeza washiriki wa mashindano hayo ya Dr. Sheni Cup ya Jimbo la Kiembe Samaki kwa umahiri waliouonyesha kwenye michezo yao ambayo imechipua vipavi vilivyochangia kuleta burdani safi kwa wapenzi waliokuwa wakifuatilia mashindano hayo.
“ Niko tayari kusaidiana na Viongozi wenu wa Jimbo katika kuona tunaboresha viwanja vyenu vya michezo hasa lile ombi lenu la kutaka kutumia kiwanja hichi hata nyakati za usiku kwa kuweka taa “ Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba hilo linawezekana kwa sababu vipo baadhi ya viwanja vinatumika wakati wa usiku   akitolea mfano wa viwanja  hivyo ambavyo tayari vipo hapa Zanzibar  kuwa ni vile vya Jimbo la Uzini na Kitope.
Hata hivyo Balozi Seif alionyesha masikitiko yake kutokana na baadhi ya watu wasiopend michezo wala maendeleo ya Nchi hii kwa uwamuzi wao wa kuiba baadhi ya taa zilizowekwa katika kiwanja cha Kitope.
Katika kuunga mkono vugu vugu la wanamichezo hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliahidi kuzichangia Jezi Seta moja , Mipira Miwili  na Shilingi 50,000/- kwa kila Timu kati ya nane zilizoshiriki mashindano hayo ya Kombe la Dr. Sheni.
Katika Fainali hiyo Balozi Seif alikabidhi zawadi ya shilingi Laki 300,000/-, Jezi seti Moja, Mipira Miwili pamoja na Kikombe kwa bimbwa wa mashindano hayo Timu ya Soka ya Small Ziko.
Mshindi wa Pili wa kombe hilo ni Timu ya Hibron aliyoikabishi zawadi ya Seti moja ya Jezi, Mipira Miwili pamoja na shilingi Laki 150,000/-, wakati Mshindi watatu Timu ya Soka ya New Generation akaikabidhi  Jezi seti Moja, Mpira Mmoja na shilingi 75,000/-.
Balozi Seif pia alimkabidhi zawadi ya shilingi 50,000/- Kamisaa wa Mashindano hayo Issa Ahmada Jogoo kwa kusimamia vyema mashindano hayo pamoja na waamuzi walioendesha mashindano hayo nao pia kuzawadiwa kitita cha fedha.
Zawadi hizo  zilikwenda sambamba na mchezaji bora  Omar Mohd, Mfungaji Bora Yunus Amour, Kipa Bora Iddi Abeid, Mchezaji mdogo kuliko wote Khamis Omar pamoja na Timu bora kuliko zote Timu ya Chukwani United ambapo kila mmoja alipata kitita cha shilingi 50,000/-.
Mapema Mbunge wa Jimbo la Kiembe Samaki Waride Bakari Jabu  amewaahidi wanamichezo hao kwamba Uongozi wa Jimbo la hilo utahakikisha kwamba mashindano hayo yanaendelezwa na kufanyika kila mwaka Jimboni humo.
Mbunge huyo alielezea faraja yake kutokana na mashindano hayo kufanyika  katika mazingira ya  amani na upendo ndani ya wiki nzima tokea kuanza kwake tarehe 16/9/2013 na kuleta burudani safi kwa wapenzi wa michezo jimboni humo na vitongoji vyake.
Mashindano hayo ya Dr. Sheni Cup ndani ya Jimbo la Kiembe Samaki yalishirikisha Timu Nane za Soka ambazo ni  Chukwani United, Kiembe Samaki United, Mbweni Academy, Hibron – Wasambaa walioibuka na Ushindi wa Pili, Small  Ziko ambao ndio mabingwa wa Kombe hilo, Mbweni Star, New Generation pamoja na Beach Boys.



Othman Khamis  Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
23/9/2013.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni