Habari

Ijumaa, 20 Septemba 2013

Zaidi ya Watu 30 Wapoteza Maisha Ajali ya Barabarani.

Na Mwashamba Juma

WATU 30 walifariki dunia katika ajali 28 za barabarani zilizotokea baina ya Mei na Agosti mwaka huu Unguja na Pemba.

Kati ya waliokufa watu 26 walikuwa wanaume na wanne wanawake.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Ziwani, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Yussuf Kija Ilembo alisema, kati ya vifo hivyo watu 11 walifariki katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja ambao wote walikuwa wanaume.

Kwa upande wa Mkoa wa Kusini Unguja Ilembo alisema watu nane walikufa katika ajali hizo miongoni mwao sita walikuwa wanaume na wanawake wawili ambapo Kaskazini Unguja watu wawili wote wakiwa wanaume walipoteza maisha.

Aidha alisema ajali hizo zilisababisha zaidi ya majeruhi 570 ambao wanaume walikuwa 300 na wanawake 270.

Miongoni mwao watu 384 wakiwemo wanaume 173 na wanawake 211 walijeruhiwa Mkoa wa Mjini Magharibi pekee, 90 miongoni mwao wanaume 62 na wanawake 28 walijeruhiwa katika Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo wengine 56 wakiwemo wanaume 38 na wanawake 18 walijeruhiwa Kaskazini Unguja.

Alisema makosa ya barabarani 6,505 yaliripotiwa katika kipindi hicho.

Aidha alisema makosa 1,226 yaliripotiwa mikoa miwili ya Pemba na makosa 4,907 yalikamatwa katika mikoa mitatu ya Unguja ambapo mkoa wa Mjini Magharibi uliongoza kwa kuwa na makosa mengi yaliyofikia 2,572.

Akizungumzia watuhumiwa wakiokamatwa kwa makosa mbalimbali ya barabarani kwa kipindi cha hicho,alisema watuhumiwa 6,681 wakiwemo wanaume 6,648 na wanawake 33 walikamatwa katika matukio hayo.

Alisema takwimu hizo zimekusanywa na polisi baada ya kumaliza wiki ya usalama barabarani inayofanyika kila mwaka ambapo kwa mwaka huu ilifanyika Aprili 22.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni