Habari

Alhamisi, 3 Oktoba 2013

Jamii Nchini inapaswa kuendelea kusaidia Jumuiya zinazojitolea


Jamii Nchini inapaswa  kuendelea  kusaidia Jumuiya zinazojitolea katika mapambano  dhidi ya maambukizo ya virusi vya Ukimwi ili kuwapa faraja na matumaini zaidi  watu ambao tayari wameshaathirika na maradhi hayo.
Makamu  wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati akikabidhi msaada wa vyakula  kwa ajili ya kuwahudumia watoto wenye mazingira magumu wanaoishi na virusi vya ukimwi ambao  wazazi wao tayari wameshafariki Dunia.
Balozi Seif alitoa msaada huo wa  Mchele, Mafuta na Sabuni uliowasilishwa na Naibu Katibu wake Nd. Suleiman Haji Suleiman  kwa Uongozi wa Kituo cha Jamii na Watoto cha Jumuiya ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar               { ZAPHA+ }  kiliopo Welezo.
Alisema msaada huo unatokana na ahadi aliyoitoa hivi karibuni ya kukubali kusaidia watoto wenye  mazingira magumu wanaoishi na virusi vya ukimwi ambao wazazi wao wameshafariki  Dunia kutokana na maradhi hayo.
Halkadhalika alieleza kwamba amepata msukumo wa kutoa msaada huo hasa ikizingatiwa kwamba siku kuu ya Iddi el Hajj inakaribia ili wapate kusherehekea vyema Siku Kuu hiyo kubwa ambayo waumini wa Dini ya Kiislamu hukusanyika Makka Nchini Saudi Arabia Kutekeleza Nguzo ya Tano ya Kiislamu kwa wale muumini mwenye uwezo.
Akipokea msaada huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Zapha+ Bibi Hasina Hamad amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa uungwana wake wa kutekeleza ahadi aliyowapa ndani ya kipindi kifupi kilichopita.
Bibi Hasina alisema msaada huo licha ya kwamba hautokidhi mahitaji ya watoto hao moja kwa moja lakini inafurahisha kuona utapunguza mzigo mkubwa uliokuwa ukiukabili Uongozi wa Jumuiya hiyo katika kuwahudumia watoto hao.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wadhamini wa Zapha+ amewaomba wananchi, wahisani na wafadhili tofauti ndani na nje ya Nchi kuendelea kuunga Mkono juhudi za Jumuiya  hiyo ili ifikie lengo la kuanzishwa kwake.
“ Tunaamini kwamba wapo watu, washirika, wahisani na hata taasisi tofauti ziwe za Kijamii na hata za ziserikali ambazo zitajitokeza kuwasaidia watoto wetu hawa tukitambua kwamba hili ni jukumu letu zote jamii “. Alifafanua Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wadhamini ya Zapha+ Bibib Hasina Hamad.
Wakati huo huo Kampuni ya Malik Food inayojihusisha na biashara ya Kuku             { maarufu  Paja nono }  imeitikia wito wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Zapha+  wa kusaidia watoto wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ambao wazazi wao wameshafariki Dunia.
Akikabidhi Boksi Mbili za Mapaja ya Kuku zenye uzito wa Kilo  20 zikiwa na thamani ya shilingi 80,000/- Mkurugenzi wa Kampuni ya Malik Food Bwana Fikirini Hango alisema uongozi wa kampuni hiyo umeamua kutoa msaada huo ili kuitikia wito wa Serikali wa kusaidia Jamii zenye kuishi katika mazingira Magumu.
Mkurugenzi Fikirini alisema licha ya Kampuni hiyo ya kuendesha biashara hiyo ya Kuku walio katika kiwango kinachokubalika lakini pia hujipangia utaratibu wa kutoa misaada kwa wananchi kulingana na mazingira ya mahitaji ya Jamii.
Akipokea msaada huo Mwenyekiti wa Jumuiya ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi Zanzibar Zapha + Bibi Consolata John aliipongheza Kampuni ya Malik Food kwa jitihada zake za kusaidia jamii hasa watoto mayatima muda wowote ule wanapoombwa kufanya hivyo.
Bibi Consolata aliikumbusha Jamii hapa Nchini kuendelea kuelewa kwamba jukumu la ulezi wa watoto wenye mazingira magumu ambao wameathirika na virusi vya ukimwi si la Jumuiya ya Zapha + pekee bali ni la Jamii yote kwa ujumla.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/10/2013.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni