Habari

Jumanne, 1 Oktoba 2013

Maalim Seif afanya Manzungumzo wa uongozi wa Chama cha Waalimu Zanzibar(ZATU).

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na viongozi wa Chama Cha Walimu Zanzibar (ZATU), Ofisini kwake Migombani.

Na Hassan Hamad OMKR
 
Chama Cha Walimu Zanzibar (ZATU), kimepongezwa kutokana na uvumilivu walionao katika kutafuta njia muafaka za kutatua kero zinazowakabili.
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, ametoa pongezi hizo Ofisini kwake Migombani, wakati akizungumza na viongozi wa  Chama hicho wakiongozwa na Rais wa ZATU, Salim Kitwana Sururu.
 
Amesema takriban nchi zote za Afrika Mashariki zimekuwa zikikumbwa na migogoro kati ya serikali na vyama vya walimu, lakini ni jambo la kufurahisha kuona Chama Cha Walimu Zanzibar hakiingi katika migogoro hiyo na badala yake kimekuwa kikitumia njia za Kidiplomasia katika kutatua kero zake.
 
Amekitaka Chama hicho kuendeleza moyo huo, kwani njia bora ya kutatua mizozo ni mazungumzo, na wala sio malumbano au migomo.
Amefahamisha kuwa uzoefu unaonesha kuwa mara nyingi inapotokea migomo ya walimu linaloathirika ni Taifa na vijana, na kwamba hakuna haja ya kushiriki au kushabikia malumbano ya aina hiyo.
 
Ameeleza kuwa Serikali kwa upande wake iko tayari kukutana na wadau mbali mbali kujadiliana juu ya kero zinazowakabili, ili kutafuta njia ya kuzitatua kwa njia ya amani bila ya kuwepo malumbano.
 
 
Kwa upande wake Rais wa Chama Cha Walimu Zanzibar (ZATU), Salim Kitwana Sururu, amesema ni heshima kubwa kwa Zanzibar kutokumbwa na migomo ya walimu ambayo imekuwa ikijitokeza katika nchi jirani mara kwa mara.
 
Ameahidi kuwa ZATU kitaendelea kutumia njia za mazungumzo katika kutatua kero zinazowakabili, na kwamba kitafanya hivyo ili kulinda heshima ya Zanzibar.
 
Naye Katibu Mkuu wa Chama hicho Mussa Omar Tafurwa, ameiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuitekeleza kikamilifu Sera ya Elimu Zanzibar, ili kuleta maendeleo yaliyokusudiwa katika sekta ya elimu.

Amefahamisha kuwa bado yapo mambo mengi ambayo hayajatekelezwa ndani ya sera ya elimu ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Mamlaka ya uajiri wa walimu, pamoja na Baraza la Walimu Zanzibar, mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni