Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Nguruweni kabla ya kuwakabidhi hati za umiliki wa mashamba ya kilimo wakulima hao.
Baadhi ya wananchi na wakulima wa Kijiji cha Nguruweni wakiwa katika mkutano maalum uliotishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa kukabidhiwa hati za umiliki wa mashamba ya kilimo katika maeneo yao.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewatahadharisha Wakulima wa Viijiji vya Ndunduke, Nguruweni na Dole kuhakikisha kwamba maeneo ya kilimo waliyokabidhiwa na Serikali kwa shughuli za Kilimo wanayatumia kama yalivyopangwa na kukubalika na pande hizo mbili.
Wakulima hao wakaonywa kuwa ye yote atakaeamua maeneo hayo kuyakata viwanja kwa ajili ya kujenga nyumba au kuyauza kwa mtu mwengine aelewe kwamba Serikali italazimika kumnyang’anya mkulima huyo mara moja.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akikabidhi hati za umiliki wa mashamba ya kilimo kwa ajili ya wakulima 40 kati ya 181 wa Kijiji cha Nguruweni waliokuwa wakiilalamikia Serikali kwa kipindi kirefu kuidhinishiwa mashamba wanayoyatumia ili kuendeleza shughuli zao za Kilimo.
Balozi Seif amesema wapo baadhi ya watu wenye tabia ya kuomba mashamba au eka kwa kisingizio cha kuendeleza kilimo lakini badala yake hujenga tamaa inayowaelekeza kuanza kukata viwanja na kuuzia watu wengine.
Balozi Seif amesifu ustahamilivu ulionyeshwa na wakulima hao na kusema kwa kiasi kikubwa umesaidia kuendeleza amani na utulivu kwenye Vijijini hivyo vya Nguruweni, Ndunduke pamoja na Dole ambayo imeleta faraja kwa Serikali Kuu kwa vile haikuathiri shughuli za kila siku za kijamii.
Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Nd. Ali Juma amesema Taasisi za Kilimo na Ardhi zililazimika kufanya uhakiki wa kina ili kuwatambua wakulima halali waliokuwa wakistahiki kupatiwa hati hizo.
Amesema uhakiki huo ulioshirikisha pia Masheha wa Vijiji vilivyohusika na mgogoro huo vya Nguruweni Ndunduke na Dole umeibua wakulima wapatao 181 ambapo wakulima 40 kati ya hao wamethibitika kupatiwa hati hizo kwa awamu ya kwanza.
Akitoa shukrani zake Mwenyekiti wa Kamati Maalum iliyounda na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozib Seif kushughulikia mgogoro huo wa mashamba ya vijiji vya Nguruweni, Ndunduke na Dole Mh. Abdulla Mwinyi amesema Wakulima wa Vijiji hivyo wanapaswa kupongezwa kwa umahiri wao wa ustahamilivu kufuatia mgogoro huo wa mashamba kwenye eneo hilo.
Hata hivyo Mh. Abdulla Mwinyi ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi amewaomba wale wakulima ambao bado mgogoro wao haujapatiwa ufumbuzi waendelee kuwa na subra kwa vile Serikali kupitia Uongozi wa Kamati hiyo unajitahidi katika kukamilisha mchakato huo.
Akitoa shukrani kwa Niaba ya Wakulima hao Mmoja wa Wazee wa Vijiji hivyo Mzee Kitwana Mustafa alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ujasiri na uungwana wake aliouchukuwa wa kutimiza ahadi aliyowapa mwaka jana wa kumalizika kwa kadia hiyo.
Mzee Kitwana alisema wakulima wa Vijiji hivyo wamefarajika na hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwatatulia kero lililokuwa likiwasumbua kwa miaka mingi iliyopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwahi kutoa ahadi kwa wakulima hao wa Nguruweni, Ndunduke na Dole kwamba Serikali itayagawa maeneo yote ambayo kamati aliyoiunda tarehe 14 Disemba Mwaka 2012 Chini ya Mwenyekiti wake Mh. Abdulla Mwinyi kufanya uhakiki wa mashamba yote yaliyoleta mgogoro.
Wakulima hao waliwahi kutoa shutuma kali kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif dhidi ya watendaji na Maafisa wanaosimamia Ardhi, Kilimo wakiwemo pia Viongozi wa ngazi ya kati wa Serikali kwa vitendo vyao vya kuingiza wakulima waliokuwa hawahusiki na mashamba hayo.
Serikali ililazimika kuzuia utolewaji wa hati hizo kufuatia hitilafu zilizojichomoza za kupandikizwa baadhi ya watu wasiohusika jambo ambalo lilisababisha mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima hao na watendaji waliopewa jukumu la kusimamia suala hilo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/10/2013.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni