Wapiganaji nchini Libya wametoa wito wa kuwateka nyara raia wa Marekani mjini Tripoli na kushambulia mabomba ya gesi , meli pamoja na ndege ili kulipiza kisasi kwa kukamatwa kwa mwanachama mwandamizi wa al-Qaeda na kikosi maalum cha jeshi la Marekani nchini Libya wiki iliyopita.
Nazih al-Ragye, ambaye anafahamika zaidi kwa jina la Abu Anas al-Liby, anatuhumiwa kuhusika katika shambulio dhidi ya balozi za Marekani mwaka 1998 nchini Kenya na Tanzania ambapo watu 224 walipoteza maisha. Alikamatwa katika mitaa ya mjini Tripoli siku ya Jumamosi na anashikiliwa katika meli ya kivita ya Marekani katika bahari ya Mediterranean.
Ujumbe uliotolewa na wapiganaji wanaofuata itikadi kali za dini ya Kiislamu nchini Libya katika mtandao wa Internet umesema kuwa Benghazi inalindwa na watu wake. Ujumbe huo umewataka Walibya kufunga njia zote za kuingia na kutoka katika mji huo na kuwakamata raia wote wa Marekani pamoja na washirika wao na kuwatumia kama karata ya kufanya majadiliano ya kuachiwa wapiganaji waliokamatwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni