Rais Bashar Assad wa Syria amesisitiza kuwa majeshi ya nchi hiyo yataendelea kupambana na makundi ya kigaidi hadi amani na utulivu itakaporejea nchini humo. Kwenye mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Spiegel la Ujerumani, Rais Assad amesema kuwa iwapo nchi za Saudi Arabia, Qatar na Uturuki zitaacha kutoa misaada ya fedha, silaha na ya kilojistiki kwa makundi ya kigaidi nchini humo, mgogoro wa Syria unaweza kutatuliwa katika kipindi cha miezi michache tu.
Akiulizwa na mwandishi wa gazeti hilo kuhusu uwezekano wa kuondoka madarakani, Rais Assad amesema kuwa, wananchi wa Syria ndio wenye jukumu la kuainisha mustakbali wa nchi yao.
Aidha Rais wa Syria alichukua fursa hiyo kusisitiza kwa mara nyingine tena kwamba majeshi ya Syria hayakutumia silaha za kemikali katika eneo la pambizoni mwa Damascus.
Ameongeza kuwa, nyaraka na ushahidi unaonyesha kuwa magaidi yanayoungwa mkono na nchi za Magharibi na hasa Marekani na nchi za Kiarabu ndio waliotumia silaha hizo za maangamizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni