NYUMBA mpya ya kisasa ya kuishi Spika wa Baraza la Wawakilishi imekamilika, anatarajiwa kuhamia hivi karibuni mara baada ya kukamilika kwa matengenezo muhimu ya miundombinu ya maji safi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema hayo wakati alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa jimbo la Mtambwe, Salim Abdallah Hamadi (CUF) aliyetaka kujua lini Spika wa Baraza la Wawakilishi atahamia katika nyumba ya kisasa iliyopo Migombani.
Aboud alisema nyumba hiyo imegharimu jumla ya Sh bilioni 1.2 ambapo asilimia 62 ya fedha hizo zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na asilimia 18 ni mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha alisema nyumba hiyo imekamilika kwa asilimia kubwa ambapo kasoro zilizopo ni tatizo la ukosefu wa maji ambapo miundombinu hiyo kwa sasa inafanyiwa marekebisho.
“Nyumba ya kisasa ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho ipo katika hatua za mwisho kumalizika isipokuwa kumejitokeza kasoro ndogo ya tatizo la maji,” alisema.
Alisema nyumba hiyo imejengwa kwa kuzingatia vigezo vyote vya nyumba zinazostahiki kuishi wakuu wa nchi.
Hata hivyo Mwakilishi wa jimbo la Wawi, Saleh Nassor Juma(CUF) alisema eneo ilipojengwa nyumba hiyo sio pazuri kwa sababu ipo barabarani ambapo utulivu unakosekana.
Akijibu swali la nyongeza la mwakilishi huyo, Aboud alisema kuwepo nyumba hiyo barabarani si tatizo kwa sababu hata nyumba anayoishi Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein ipo barabarani jirani na nyumba hiyo eneo la Migombani.
CHANZO- http://www.gumzolajiji.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni