Habari

Jumapili, 20 Oktoba 2013

Wapinzani waachwa solemba

 Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amesema Serikali haikusudii kufanya marekebisho yoyote kwenye Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni.

Chikawe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, ambapo alifafanua kuwa isipokuwa kama kuna watu kutoka katika taasisi ambazo zina mapendekezo yao wanayoona ni vyema yaingizwe kwenye sheria hiyo, wanatakiwa kufuata utaratibu unaotakiwa ili kufanikisha.
“Serikali haina marekebisho yoyote ila najua kuna vyama vya siasa vinakutana na vinakusanya mapendekezo yao, naamini kwamba watafuata taratibu zinazotakiwa ili marekebisho wanayopendekeza yaweze kuingizwa kwenye sheria hiyo.
Awali mwenyekiti wa mchakato shiriki wa vyama vyenye wawakilishi bungeni, James Mbatia alieeleza kuwa wapo katika hatua nzuri ya majadiliano ambayo yanalenga katika kupambana na changamoto kwenye sheria hiyo.
“Nakuhakikishia mwandishi kwamba kuna ushirikiano mzuri miongoni mwa vyama vyote vinavyoshiriki katika mchakato huo, tunaangalia makosa yaliyojitokeza na kuzusha changamoto ni mchakato wa kupata Katiba Mpya, tutakutana tena siku ya Jumapili baada ya hapo tunazungumza na vyombo vya habari tupeni muda kwanza,” alisema Mbatia.
Alivitaja vyama vinavyoshiriki katika mchakato huo kuwa ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), NCCR-Mageuzi, Chama cha Dekmokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Labour Party (TLP) Chama cha Wananchi (CUF) na United Democratic Party (UDP).
Waziri Chikawe kabla ya mswada kusainiwa na Rais Kikwete aliwahi kuonya kuwa muswada huo ukirudi bungeni bila kusainiwa unaweza kusababisha vurugu kubwa zaidi ya zile za mara ya kwanza kutokana na tofauti kati ya wabunge wa CCM na wale wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.
Rais Kikwete, alisaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba Mpya 2011, uliopitishwa na Bunge mjini Dodoma, Novemba 18 mwaka huu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni