Habari

Ijumaa, 4 Oktoba 2013

Tutaishia kumnunua Tambwe tu

MWISHONI mwa miaka ya themanini, kiongozi mmoja wa Simba alisimama katika ngazi ya mwisho katika mlango wa kuingia ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), akawageukia mashabiki waliokuwa wamemsindikiza uwanjani hapo akiwaonyesha Briefcase aliyokuwa ameibeba kwa ajili ya kwenda kumsajili, John Makelele ‘Zig Zag’ jijini Mwanza.
Kwa mbwembwe alitabasamu. Akageuka zake akaingia ndani ya ndege. Haikuchukua saa 24, tayari alikuwa amemaliza kumsajili Makelele. Akarudi kwa mbwembwe. Sasa nasikia jamaa hana kitu. Briefcase lake haina hata Sh1,000.
Lakini nani anajali? Watu wanamwangalia anayesajili wachezaji wa sasa. Mambo ya Makelele yalishapita. Watu wanaangalia nani amemleta Hamis Tambwe. Wanaangalia nani amemleta Betram Mwombeki. Ndivyo maisha ya Simba na Yanga yalivyo.
Hata sasa najiuliza. Katika hizi kelele za viwanja vyao wanavyofikiria kujenga, ni nani hasa ana moyo wa kwenda benki na kukopa kwa niaba ya Yanga?
Karibu kila kiongozi ana shughuli zake. Huyu ni Mwanasiasa, yule ni mfanyabiashara bilionea, yule mwingine ni Mwandisi, yule pale ni bosi wa benki. Hakuna ambaye maisha yake yanategemea timu.
Kwa nini akubali kufanya miradi ya maana ya muda mrefu kwa ajili ya klabu? Hasa akigundua kwamba anawafanyia watu wasio na shukrani ambao pia wanaweza kumtukana kama mtoto mdogo?
Unamkumbuka yule tajiri aliyeenda kusuluhisha matatizo ya Yanga? Ghafla akatokea mtu mmoja ana kandambili zenye rangi mbili tofauti. Ya kushoto ina rangi ya njano, ya kulia ina rangi ya kijivu. Lakini akamtukana matusi ya nguoni tajiri yule pamoja na familia yake. Yule tajiri hajakanyaga Jangwani tena.
Unafikiri wanaoongoza klabu hizi hawana akili? Wanazo. Wanachofanya ni kujaribu kupitisha muda wao waondoke huku wakifanya mipango ya muda mfupi. Kila mmoja hana uhakika na maisha yake klabuni.
Hizi simulizi za ujenzi wa viwanja huwa nazisikiliza kwa sikio la ujanja ujanja tu. Kinachoweza kufanyika kwa sasa ni kuhakikisha timu inamilikiwa na watu wenye maslahi ya moja kwa moja klabuni. Wengine tubakie mashabiki.
Florentino Perez anapomnunua Cristiano Ronaldo kwa Pauni 80 milioni, hafanyi kwa ajili ya kuwafurahisha mashabiki. Tayari anakuwa ameshapigiwa hesabu za biashara na timu yake ya watu wa masoko. Faida inakwenda katika mfuko wa klabu na yeye mwenyewe binafsi kama mmiliki wa klabu.
Tunahitaji timu zetu ziingie katika mfumo huu. Ziingie katika soko la hisa. Mwenye hisa nyingi ndiye mmiliki wa klabu. Hata akifa, mwanaye anaweza kuongoza klabu. Mpaka atakapojitokeza tajiri mwingine wa kununua hisa zake.


Ni hapo ndipo mtu anaweza kuwa ‘bize’ na ujenzi wa uwanja. Anajua baadaye kuna faida kubwa itaangukia kwake binafsi. Lakini hapa tunajidanganya kuwa Mwenyekiti inabidi afanye kazi ya Kanisa au Msikiti. Hana mshahara klabuni, hana biashara klabuni, hana hisa klabuni.
CHANZO-MwanaSpoti

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni