By DORIS MALIYAGA
- Mazoezi hayo yalihusisha programu tofauti zaidi ikiwa ni kujenga ukakamavu. Kuhusiana na mazoezi hayo, Brandts aligoma kuweka wazi kama amegundua chochote kwenye kikosi chake katika mechi zilizopita.
KOCHA wa Yanga, Ernest Brandts, amehamishia kikosi hicho kwenye mazoezi ya gym akisema timu itakuwa huko kwa mwezi mzima.
Hata hivyo katika mazoezi hayo, wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza; Wanyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, Mbuyu Twite na Mrundi Didier Kavumbagu hawakutokea kutokana na sababu mbalimbali.
Kwenye mazoezi hayo yaliyoanza Jumatatu, Athuman Idd ‘Chuji’ alitinga na mwanaye anayeitwa, Sabri, ambaye alimwacha kwenye kochi akipiga usingizi wakati yeye akijenga misuli.
Mazoezi hayo yalihusisha programu tofauti zaidi ikiwa ni kujenga ukakamavu. Kuhusiana na mazoezi hayo, Brandts aligoma kuweka wazi kama amegundua chochote kwenye kikosi chake katika mechi zilizopita.
Akizungumza na Mwanaspoti, Brandts alisema leo Alhamisi watarejea uwanjani kama kawaida kujiandaa na mechi ya Mtibwa Sugar Jumapili.
“Kwenda gym ni sehemu ya programu yetu tuliyojipangia ambayo huwa naandaa ndani ya mwezi mzima. Malengo ni kuweka timu fiti ikabiliane na hali yoyote watakayokutana nayo kwenye mechi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mbuyu hajaonekana kwenye mazoezi ya kikosi hicho kuanzia juzi Jumanne. Niyonzima hajafika kwa siku mbili wakati Kavumbagu ni siku moja.
Mwanaspoti iliwatafuta wachezaji hao. Niyonzima alisema: “Sikuwa najisikia vizuri ingawa kwa sasa naendelea vizuri na nategemea kesho (leo Alhamisi) kuanza pamoja na wenzangu.”
Kavumbagu alisema: “Sijikii vizuri, siko sawa tu ila nategemea kuanza kesho (leo Alhamisi) na wenzangu naona naendelea vizuri kwa sasa.”
Daktari wa Yanga, Nassor Matuzya alisema: “Sijui matatizo yao kwani kama yangekuwa yanahusu ugonjwa ningejua, lakini kinachowasumbua kwa sasa sikijui na sina taarifa nao.”
Brandts naye alisema, hana taarifa nao na anachojua jana Jumatano wangekuwa kwenye mazoezi ya timu kauli iliyoungwa mkono na meneja, Hafidh Saleh, naye akisema hana taarifa nao.
CHANZO-MWANASPOTI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni