JESHI la Polisi mkoni Kilimanjaro limemnasa mtuhumiwa muhimu aliyekuwa akitafutwa kwa muda sasa anayedaiwa kupanga mauaji ya bilionea wa madini ya tanzanite, marehemu Erasto Msuya (43), aliyeuawa kwa kupigwa risasi mwezi Agosti, mwaka huu.
Mtuhumiwa huyo aliyetajwa kwa jina la Alli Musa (42) maarufu kama ‘Majeshi’ alikamatwa mkoani Kigoma akijaribu kutorokea nchini Burundi baada ya kufanikiwa kukimbia mitego ya polisi katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Mwanza.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na tayari amefikishwa mkoani hapa na kuhojiwa na makachaero wa Jeshi la Polisi kabla ya kuunganishwa na wenzake katika kesi ya mauaji ya kukusudia.
“Ni kweli kuna mtu huyo tunamshikilia baada ya kukamatwa wiki iliyopita huko Kigoma na tunamhoji ili kukamilisha upepelezi na utakapokamilika ataunganishwa na wenzake katika kesi ya msingi inayowakabili,” alisema Boaz.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ambaye pia anadaiwa amewahi kulitumikia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)kabla ya kufukuzwa kunabadili sura ya kesi hiyo na kufanya idadi ya watuhumiwa kufikia wanane.
Washitakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Sharif Mohamed Athuman (31) mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredi (38), mkazi wa Songambele Wilaya ya Simanjiro na Mussa Juma Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu mkoani Arusha.
Wengine ni Joseph Damas Mwakipesile maarufu kama Chusa (36), mfanyabiashara wa madini na mkazi wa Arusha, Jalila Zuberi Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Mohammed Jabir a.k.a ‘Msudani’ au ‘Mnubi’(32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata wilayani Hai na Karim Kihundwa (33) mkazi wa Kijiji cha Lawate Wilaya ya Siha.
Mfanyabiashara Erasto Msuya aliuawa Agosti 7, mwaka huu majira ya 6:30 mchana kwa kupigwa risasi 13 kifuani, kando ya barabara kuu ya Arusha– Moshi katika eneo la Mjohoroni, Wilaya ya Hai, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
CHANZO-TANZANIA DAIMA
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni