Taasisi tano za Kiislamu za nchini Myanmar zimeiomba serikali kuwalinda Waislamu nchini humo kufuatia kuzuka tena mauaji dhidi yao katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia.
Katika taarifa yao ya pamoja, taasisi hizo zimesema: "Tunaiomba serikali ihakikishe utawala wa sheria unaheshimiwa nchini humo na Waislamu tunalindwa."
Polisi wa nchi hiyo wamesema leo kuwa, Waislamu wasiopungua watano, yaani wanaume wanne na mwanamke mmoja wameuliwa katika kijiji cha Thabyuchaing baada ya kijiji hicho kuvamiwa kikatili na mamia ya wafuasi wa dini ya Kibudha.
Shambulio kama hilo lilitokea pia jana kwenye eneo la Thwande katika jimbo la Rakhine baada ya zaidi ya Mabudha 700 kuvamia mitaa ya mji huo.
Bikizee mmoja aliuawa na makumi ya nyumba za Waislamu zilichomwa moto hiyo jana. Karibu Waislamu 140,000 wengi wao wakiwa ni wa kabila la Rohingya wamepoteza makazi yao katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar.
Mamia ya Waislamu wa Myanmar wameuawa tangu mwaka 2012 baada ya wafuasi wa dini ya Kibudha kushadidisha mashambulizi yao dhidi ya Waislamu hao wasio na ulinzi.
CHAZO-IDHAA YA KISWAHILI YA IRAN.
Alkhamisi, 03 Oktoba 2013 08:46
UN yataka misaada ya kibinadamu ipelekwe Syria
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka pande zote zinazohusika katika mgogoro wa Syria zisaidie kurahisisha upelekaji misaada ya kibinadamu katika nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na baraza hilo imezitaka pande zote husika katika mgogoro huo kusaidia mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa na ya kujitegemea kuchukua hatua za haraka za kuwezesha upanuzi wa operesheni za misaada ya kibinadamu.
Pia pande zote zimetakiwa kuwahakikishia usalama maafisa wa Umoja wa Mataifa na wahudumu wa misaada ya kibinadamu.
Hivi karibuni Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilitangaza kuwa, idadi ya wakimbizi wa Syria waliokimbia mapigano nchini humo imefikia milioni mbili. Pia karibu watu milioni 4.5 wameyakimbia makazi yao ndani ya Syria tangu mgogoro wa nchi hiyo ulipoanza na wanahitajia misaada.
CHAZO-IDHAA YA KISWAHILI YA IRAN.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni