Habari

Ijumaa, 6 Desemba 2013

Lissu: Muswada wa kura za maoni ni kinyume cha Katiba

Dodoma.Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni imetaka Muswada wa Kura ya Maoni uondolewe bungeni hadi hapo Bunge litakapofanya marekebisho ya Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa unapingana nayo.


Awali, muswada huo ulikuwa ujadiliwe katika Mkutano wa 12 wa Bunge lakini uliahirishwa kutokana na wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge wanaotoka Zanzibar kupinga vikali kura ya maoni kupigwa visiwani humo kwa kuwa tayari huko kuna sheria hiyo.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jana, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu alisema katika Katiba ya sasa, hakuna mahali ambako kura ya maoni inatajwa.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema tofauti na Katiba ya Jamhuri, Katiba ya Zanzibar imetambua kura ya maoni kwa kuitaja rasmi katika Katiba na kuiwekea utaratibu.
“Kwa maoni ya kambi ya upinzani, Serikali ya CCM inaogopa kufungua mjadala wa marekebisho ya Katiba ili kuruhusu kura ya maoni kwa hofu kuwa mjadala huo, utapanuliwa kwa kuhoji uhuru wa Tume ya Uchaguzi katika kuendesha na kusimamia uchaguzi,” alisema.
Alisema hofu ya CCM haiwezi kukubaliwa na Bunge kama sababu ya msingi ya kutunga sheria ambazo zinapingana na Katiba.
“Kwani kwa kufanya hivyo itakuwa sawa na kubariki ukiukwaji wa Katiba ambao wabunge wote tuliopo ndani ya ukumbi huu tuliapa kuhifadhi, kuilinda na kuitetea,” alisema Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni.
Awali, akiwasilisha muswada huo bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Waziri Mkuu), Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema: “Ili kuepuka mkanganyiko unaojitokeza iwapo sheria za uchaguzi zilizopo zitatumika kusimamia uendeshaji wa kura ya maoni, Serikali imeona umuhimu wa kutumia kura ya maoni kwenye mchakato wa kutunga Katiba Mpya.
“Sheria hii si ya kudumu na itafikia ukomo wake, mara tu baada ya Katiba Mpya kupatikana na haya ndiyo madhumuni makuu ya kupendekeza kutungwa kwa sheria hii ya kura ya maoni,” alisema.
Alisema mpigakura aliyesajiliwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), au Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), atakuwa na haki ya kupiga kura ya maoni.
Kamati
Kwa upande wake, Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, imeshauri muda wa kukata rufaa kuongezwa hadi siku saba badala ya tano zilizopendekezwa katika muswada huo. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pindi Chana alisema Ibara ya 45 ya muswada huo, inaweka masharti kwa kamati ya kura ya maoni ambayo haikuridhika na uamuzi wa mahakama ya chini, kuwasilisha rufaa yake ndani ya siku tano tangu tarehe iliyopata nakala ya hukumu.
Kamati hiyo pia imeshauri Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lianze kuboreshwa kwa sababu vijana wengi wamefikisha umri wa kupiga kura na hawajaandikishwa.
Chana alisema kamati inaunga mkono mapendekezo ya muswada huo kuwa kura zitangazwe ndani ya saa 72 tangu kufungwa kwa vituo vya kupigia kura.
“Kamati inashauri Serikali kuandaa vifaa vya kisasa na kuwajengea uwezo watendaji wa tume zote mbili ili waweze kumudu usimamizi wa mchakato wa upigaji wa kura ya maoni kwa weledi na umahiri wa hali ya juu,” alisema. Aidha, alisema kamati inaunga mkono mapendekezo ya muswada huo kuwa matokeo ya kura ya maoni yataamuliwa kwa kigezo cha asilimia 50 ya kura halali zilizopigwa za kuunga mkono swali la kura ya maoni kwa pande zote mbili za Muungano.
“Ibara ya 34(2) inaweka sharti la wingi wa kura halali zilizopigwa katika suala la kura ya maoni kuwa ndilo litakaloamua kuhusu kukubalika au kutokukubalika kwa katiba inayopendekezwa. Kamati inaunga mkono masharti haya kwa kuwa uamuzi wa wananchi ndiyo wa mwisho kuhusu jambo kubwa na nyeti kama la Katiba,” alisema Chana.
Wabunge Z’bar wapinga
Utaratibu wa kuwatumia masheha katika uandikishaji wa vitambulisho vya ukaazi Zanzibar umezua mjadala mkali bungeni baada ya wabunge wa CUF, kupinga kutumika katika kuwapata wapiga kura wa Katiba Mpya.
Akichangia Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013, Mbunge wa Chakechake, Mussa Haji Kombo alitaka kufutwa kwa kipengele kinachotaka kutumika kwa Daftari la Wapiga Kura la Zanzibar katika kupiga kura za maoni kwa kuwa kitawanyima haki Watanzania ambao hawakuandikishwa kutokana na kunyimwa vitambulisho vya ukaazi na masheha.
“Msitugawe kwa kutubagua, leo hii mtu anayeandikishwa Tabora (katika daftari la wapiga kura) haulizwi kitambulisho cha ukaazi lakini wa Micheweni haandikishwi bila kuwa na kitambulisho cha ukaazi,” alisema. “Kuna danadana nyingi katika uandikishaji wa vitambulisho vya ukaazi lakini watoto wa miaka 12 wa wanachama wa CCM wameshapata vitambulisho… zoezi hili ni muhimu tutaliharibu kwa kufuata matakwa ya vyama,” alisema Riziki Omary Juma (Viti Maalumu).
Mbunge wa Mkoani, Ally Khamis Seif, alishauri kuanzishwa kwa daftari lingine la wapiga kura ambalo halitahusisha masharti ya kuwa na vitambulisho vya ukaazi ili kuwapa nafasi Wazanzibari wote kupiga kura katika mchakato huo.
“Kama mimi Sheha wangu wa Konde alininyima kitambulisho cha ukaazi kama ya Mbunge yamekuwa hayo je, Watanzania wa kawaida? Hili jambo litatuletea taabu katika maamuzi haya magumu tunayoyafanya, tuache kutumia daftari la wapiga kura la Zanzibar lile si daftari lile ni uchochezi litatuletea taabu,” aliongeza Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji.
Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni