Na Shemsia Khamis, PEMBA
MAHAKAMA ya Mkoa Chakechake, chini ya Hakimu Khamis Ramadhan Abdalla, imempandisha kizimbani mshtakiwa Abuu Said Omar (15), mkaazi wa Wawi Chakechake, kujibu tuhuma za kumlawiti mtoto wa kiume (14), zilizomkabili mahakamani hapo.
Ilidaiwa mahakamani hapo, na Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar,Ali Bilali Hassan kuwa, mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo, Machi 14 mwaka huu majira ya saa 7:00 mchana.
Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa, mshtakiwa alimuingilia mtoto huyo kinyume na maumbile, katika mabonde ya Wawi Mtega, wilaya ya Chakechake.
Baada ya mshtakiwa huyo, kusomewa shitaka lake, alikana na kuiyomba mahakama impatie dhamana, kutokana na kuwa ni haki yake ya kisheria.
Kufuatia ombi hilo, Mwendesha mashtaka hakuwa na pingamizi yoyote endapo mshtakiwa ataweza kutimiza masharti ya dhamana atakayopewa na mahakama.
Hakimu aliyataja masharti ya dhamana, kuwa ni pamoja na yeye binafsi kujidhamini shilingi milioni 2,000,000 za maandishi na wadhamini wawili, kima kama hicho za maandishi.
‘’Mshtakiwa wadhamini wako wawe na vitambulisho vya uzanzibar ukaazi na barua za sheha katika shehia wanazoishi ndipo tuweze kukupa dhamana’’, alisema Hakimu.
Kwa mujibu wa sheria kufanya hivyo, ni kosa kinyume na kifungu cha sheria cha 150 (a), sheria namba 6 ya mwaka 2004, sheria ya Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni