Habari

Jumatatu, 27 Oktoba 2014

Mawaziri Zanzibar wapigia kampeni kura ya ndiyo


Wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakishangilia jambo wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.AliMohamed Shein (hayupo pichani) alipokuwa anatoa hotuba kwa wanachama wa chama hicho.
Zanzibar.                                                                                                                                                                          Mawaziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wameanza kampeni kuwataka wananchi kuunga mkono Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa wakisema imezingatia masilahi ya Zanzibar kiuchumi na kiutawala.
Walisema hayo jana walipokuwa wakihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja. Mkutano huo ulihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein,
Makamu wa Pili wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir, Waziri wa Makazi, Ardhi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdallah Shaaban, Waziri wa Fedha wea Muungano, Sada Mkuya Salum na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan.
Katika hotuba yake, Haji alisema kwa mujibu wa Katiba Inayopendekezwa, mamlaka ya ugawaji wa mipaka ya wilaya na mikoa Tanzania Bara na Zanzibar yatabakia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isipokuwa kwa eneo la Zanzibar kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar.
Alisema Zanzibar haijapoteza mamlaka yake ya kiutawala na viongozi wa Serikali za Mitaa (Masheha), wataendelea kuteuliwa na wakuu wa mikoa na kutekeleza majukumu yao chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waziri Haji alisema, wakati ukifika watafanya kampeni wadi kwa wadi, nyumba kwa nyumba na kitanda kwa kitanda ili kuhakikisha Katiba hiyo inapitishwa kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
Waziri Mkuya alisema, ikiwa Katiba Inayopendekezwa itapitishwa, itaondoa malalamiko ya kero za Muungano na kuwataka wananchi kuiunga mkono.
Alisema Kifungu cha 262 (2), kimeeleza mamlaka ya kutoza kodi yasiyokuwa ya Muungano yatakuwa chini ya Zanzibar na mapato yake yatakusanywa na kuingizwa katika Mfuko wa Hazina wa Zanzibar na Serikali ya Muungano itaendelea kukusanya mapato katika vyanzo vyake vya mapato vya Muungano.
Waziri huyo wa Fedha alisema Katiba Inayopendekezwa itafungua milango ya kiuchumi kwa vile Zanzibar itapata nafasi ya kukopa katika taasisi za fedha pamoja na kujiunga katika taasisi za kikanda na jumuiya za kimataifa.
“Tayari Serikali ya Zanzibar na Muungano zinatayarisha mkakati wa pamoja wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini ili tuwe na waraka mmoja tu utakaotumika kutafuta mikopo ya nje,” alisema.
Suluhu alisema mfumo wa kugawana nafasi za uongozi kama vile Spika kutoka Bara na Naibu Zanzibar kama inavyopendekezwa utasaidia kuondoa malalamiko ya upande mmoja kushikilia nafasi nyingi za uongozi.
Alisema Kifungu cha 150 (4) kimesema Spika akitoka bara na Naibu wake atoke Zanzibar na alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuondoa malalamiko ya pande mbili za Muungano.
Chanzo: Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni