Mbio za urais ndani ya CCM zimechukua sura mpya baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba kutangaza rasmi kumuunga mkono mtoto wake, January Makamba.
Akizungumza katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Tegeta, Dar es Salaam, Mzee Makamba alisema ameamua kumuunga mkono January kwa sababu anaamini mwanaye ana uwezo.
“Mbali ya kwamba January ni mwanangu, lakini najua ana uwezo, anajua shida za Watanzania kwa kuwa alikuwa msaidizi wa Rais Jakaya Kikwete ambaye walizunguka naye Tanzania na dunia nzima.
“Makamba ni msomi, kijana na Tanzania ya sasa inahitaji rais wa kisasa atakayekwenda na kasi ya dunia na Junuary ni kizazi cha digitali, siyo kizazi cha BBC yaani Born Before Computer ambao hawana uwezo wa kukabiliana na kasi ya dunia ya leo,” alisema.
Mzee Makamba alisema ameamua kufunguka kuhusu msimamo wake huo, baada ya watu wengi kumuuliza anamuunga mkono nani kati ya wagombea waliotangaza nia na ambao bado hawajatangaza.
Alitoa mfano wa mti wa mkomamanga kuwa huzaa komamanga na kwamba yeye atamuunga mkono mtoto wake badala ya mtu mwingine.
Huku akitumia maneno ya kwenye Biblia alisema: “Bwana Yesu aliwahi kusema bora kuwa moto kuliko kuwa vuguvugu, maana ukiwa vuguvugu nitakutema.”
Alisema kutokana na mfano huo, ameamua kuwa moto kwa January kwa sababu haiwezekani amwache mtoto wake halafu amshabikie jirani.
Kuhusu kwa nini alichelewa kutoa tamko la kumuunga mkono January, Mzee Makamba alisema hivi karibuni mwanaye akiwa nje ya nchi alitangaza nia ya kuwania urais, kitu ambacho kilimshangaza kwa sababu hakuwa amempa taarifa.
Aliporudi alimfuata nyumbani na kumweleza nia yake hiyo, lakini walipomuuliza kwa nini amewaambia baada ya kuwa ametangaza nia yake, alisema majibu ya January yalikuwa ni kwamba, hakupenda wazazi wake wamkatalie mapema kwa sababu anaamini anaweza.
Mzee Makamba alisema, binadamu yeyote anayetaka uongozi huwa anajitathmini kwa njia tatu, kwanza anavyojijua mwenyewe, pili wanavyomfahamu wenzake na tatu kwa jinsi Mungu alivyompangia.
Katibu Mkuu huyo mstaafu wa CCM alisema kwa maana hiyo, hakuwa na sababu ya kumkatalia na akampa baraka zote.
Alimsifia baba mzazi wa Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangalla ambaye aliambatana na mwanaye siku alipotangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM Dar es Salaam.
“Mzee Kigwangalla (Nasser Kigwangalla) siku mwanaye anatangaza kuwania urais nilimwona alikuwapo na alitoa neno pale, nilifurahi sana, amenipiga bao, maana mwanangu mimi ametangazia ng’ambo, lakini sasa niko naye bega kwa bega katika harakati zake,” alisema na kuongeza: “Siwezi kukaa kimya bila ya kutoa neno wakati mwanangu ametangaza nia ya kugombea urais.”
Makamba ambaye mbali ya kuwa Katibu Mkuu wa CCM amewahi pia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro na Kigoma, alisema amewapongeza viongozi na wana CCM waliojitokeza kumuunga mkono January katika kuusaka urais.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni