Habari

Jumanne, 21 Oktoba 2014

WANANCHI WAITIKIA VYEMA ZOEZI LA CHANJO YA SURUA NA RUBELA KISIWANI PEMBA.


 Watoa huduma ya Chanjo ya Surua na Rubela wakiendelea na kazi huko Tumbe Wilaya ya Micheweni Pemba.
Na Fatma Haji-Pemba.                                                                                                                                        Zoezi la Chanjo ya Surua na Rubela limetajwa kuendelea vizuri katika maeneo tofauti ya kisiwa cha Pemba.
Akizungumza na Zenj FM Sheha wa shehia ya Uweleni Abdalla Omar Mjawiri amesema kuwa katika shehia hiyo idadi kubwa ya watoto wameshapatia chanjo hiyo na waliobakia ni wachache na itakapofika tarehe 24 watakuwa wamekamisha kwa asilimia 100 ya watoto wanaotarajiwa.
 
Amesema kuwa katika shehia ya Uweleni watoto waliotarajiwa kupatiwa chanjo hizo si zaidi ya mia saba(700)lakini katika siku 2 za kwanza  watoto zaidi ya mia tano(500)walishapatiwa chanjo hizo.
Amesema muitikio wa wazazi katika chanjo hiyo ni mkubwa uliosababishwa na uhamasishaji uliofanywa na uongozi wa shehia kwa kufanya mikutano mbali mbali ya jamii.
Akizungumzia maendeleo ya chanjo katika siku nne za kwanza  na Sheha wa Wara wilaya ya Chake Chake Gharoub Rashid amesema zoezi hilo limeitikiwa vyema na wazazi na walezi wa shehia hiyo.
Amesema licha ya kuwepo kwa changamoto kidogo ambazo alidai ni za kawaida zoezi hilo limekwenda kama llivyopangwa na kwa sasa wanamalizia kupita majumbani kuangalia kama wapo ambao hawakuweza kupata chanjo katika siku za kwanza ili wapatiwe chanjo hizo.

Kwa upande wake sheha wa shehia ya Ng`ombeni Subira Mbaraka Moh`d ametoa wito kwa wananchi ambao hawaja wapeleka watoto wao kutumia muda uliobakia kwa kuwapeleka kupatiwa Chanjo watoto wao.
Alisema wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakaidi kwa kila kitu hivyo wanaendelea na kuwahamasisha ili watoto wao wapate fursa hiyo ya chanjo zitakazowakinga na maradhi mbali mbali.
Zoezi la Chanjo ya Surua na Rubela leo li aingia katika siku ya nne na linatarajiwa kukamilika tarehe 24 mwezi huu nchini kote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni