DAWA za aina mbali
mbali za kutibu maradhi ya malaria zimeibiwa na kuisababishia serikali hasara
ya mamilioni ya shilingi.
Dawa hizo zimeibiwa katika bohari kuu ya dawa ya Mnazimmoja na kuuzwa jijini
Dar es Salaam.
Wizi huo unahusisha
kufanywa na Mtunza ghala wa bohari hiyo ambae tayari amekamatwa na kufikishwa
mahakamani.
Akiwa mbele ya mahakama ya Mkoa Vuga, mshitakiwa huyo Haji Abdallah Juma (47)
mkaazi wa Chukwani wilaya ya Magharibi Unguja, alidaiwa kuiba dawa hizo
zinazokisiwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 89.6 na kuziuza
katika duka la kuuzia dawa baridi la MIGODA OTC liliopo Kurasini wilaya ya
Temeke jijini Dar es Salaam.Mshitakiwa alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu,
Mohammed Ali Mohammed, ambalo alilikana.
Mtunza ghala huyo, alishtakiwa pamoja na mmiliki wa duka la MIGODA OTC, Khamis
Salum Kulanga (43) ambaye alisomewa shitaka la kupokea na kupatikana na mali ya
wizi.
Mashitaka hayo yaliwasilishwa na Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi
wa Mashtaka, Abdallah Mgongo.
Awali wakilili wa serikali alimsomea, mshitakiwa wa kwanza shitaka la wizi wa
mali ya serikali.
Alidai kinyume na vifungu vya 267 (1) (2) (4) na 274 (1) vya sheria namba 6 ya
2004 sheria za Zanzibar, mshitakiwa aliiba dawa aina mbali mbali za kutibu
maradhi ya malaria zinazokisiwa kuwa na thamani ya shilingi 89,625,000.
Wizi huo alidaiwa kuufanya wakati akiwa ni mtunza ghala mkuu wa bohari kuu ya
dawa iliyopo Mnazimmoja wilaya ya Mjini Unguja.
Dawa alizodaiwa kuziiba ni boksi 14 za Artequick, boksi 10 za Du-Cotexin,
Artemether injection miligramu 80 boksi 25 na boksi 25 za Artenether injection
miligramu 40.
Pamoja na shitaka hilo wakili wa serikali chini ya kifungu cha 113 (1) (2) cha
sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, alimsomea mshitakiwa huyo shitaka la
kuisababishia hasara serikali.
Katika shitaka hilo, alidai kwamba akiwa mtunzaji ghala mkuu wa bohari ya dawa,
wakati akifanyiwa ukaguzi kwenye bohari hilo iligundulika kuwepo upungufu wa
dawa za kutibu malaria na kuisababishia hasara serikali ya shilingi 89,625,000.
Matukio yote hayo alidaiwa kuyafanya Agosti hadi Oktoba mwaka jana hapo katika
bohari kuu la dawa Mnazimmoja mjini Unguja.
Sambamba na mshitakiwa huyo, wakili wa serikali alimsomea mmiliki wa duka la
MIGODA OTC shitaka la kupokea na kupatikana na dawa hizo ambazo ni za wizi.
Aliiambia mahakama Novemba 14 mwaka jana, huko Kurasini katika duka lake la
kuuzia dawa baridi liitwalo MIGODA OTC, alipatikanwa na dawa aina ya ARTEQUICK
za kutibu malaria ambazo ni mali ya SMZ.
Hata hivyo, pamoja na kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa hao waliyakana mbele
ya hakimu na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi tayari umeshakamilika.
Hata hivyo, uliiomba mahakama iiahirishe kesi hiyo kwa ajili ya kutajwa ili
waweze kupata muda wa ziada wa kupitia jalada la kesi hiyo.
Hakimu Mohammed aliwataka washitakiwa hao kujidhamini kwa bondi ya shilingi
500,000 kila mmoja, pamoja na kuwasilisha wadhamini wawili kila mmoja ambao
kila mmoja alitakiwa kusaini bondi ya kiwango kama hicho cha fedha.
Sambamba na masharti hayo, wametakiwa kuwasilisha barua za Sheha wa shehia
wanazoishi pamoja na vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 16 mwaka huu kwa kutajwa na washitakiwa
wapo nje baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni