11/09/2013. WANANCHI
wa Vijiji vya Tironi na Kionwa shehia ya Mbuguani Wilaya ya Mkoani Pemba,
wameiomba Serikali kuwatengenezea barabara yao kwa kiwango cha lami, ili
kuwaondoshea usumbufu wanaoupata kwa muda mrefu sasa.
Wakizungumza na Sauti ya Istiqama baadhi ya wananchi hao wamesema wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa kutokana na
ubovu wa barabara hiyo, jambo ambalo linawakatisha tamaa ya kufikia maendeleo
kwa haraka.
Ali Mohamed Ali mmoja wa wananchi hao amesema usumbufu
zaidi wanaupata wakati wa kipindi cha mvua, ambapo barabara hiyo inakuwa
haipitiki kutokana na matope na madimbwi yanaoyotuwama maji huku wakisema hiyo
ndiyo njia ambayo huitumia kwa shughuli zao mbali mbali.
Amesema kukosekana kwa barabara ya uhakika kijijini
kwao, wamekua wakikosa mambo kadhaa ya lazima ikiwa ni pamoja na huduma ya
matibabu na hata majia safi na salama, ambapo suluhu ya hayo ni kuwepo kwa
barabara ya kudumu.
Naye Kassim Adam Makame, mkaazi wa kijiji hicho, amesema
kuwa, kijiji chao ni moja kati ya vijiji ambavyo vinazalisha zao la karafuu kwa
wingi katika Wilaya ya Mkoani, hivyo
barabara hiyo itakapotengenezwa itawanufaisha wao na serikali kwa ujumla.
Akizungumzia juu kadhia ya wananchi hao, Afisa
Mdhamini wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Pemba, Hamad Ahmed Baucha,
amesema kuwa Wizara yake, imo katika hatua za mwisho za kutiliana saini ya
ujenzi wa matengenezo makubwa kwa barabara hiyo kupitia Mfuko wa barabara.
Amesema wakati wowote mara zoezi hilo
litakapokamilika hatua za kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha kifusi itaanza,
ili kuwapunguzia adha na kero ya usafiri wananchi wa vijiji vya Tironi na
Kionwa shehia ya Mbuguani.
Barabara hiyo kwa sasa iko katika hatua ya kifusi
kwa baadhi ya maeneo ina urefu wa zaidi
za kilomita nne kutoka barabara kuu Mkoani -Chake.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni