Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema jitihada za kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya ugonjwa wa UKIMWI nchini hazina budi ziende sambamba na vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine ambavyo ni miongoni mwa vyanzo vya ugonjwa huo.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Kituo cha Jamii na Watoto huko Welezo Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo Dk. Shein amesema imebainika kuwa maambukizi mapya ya virusi vya ugonjwa huo kwa vijana yanahusishwa na matumzi ya madawa ya kulevya.
Dk. Shein amewaeleza wanachama wa ZAPHA+, wananchi na wageni waliohudhuria hafla hiyo kuwa tangu ugonjwa huo ulipogunduliwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikifanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuhakikisha Zanzibar haipati maambukizi mapya na pia kuondosha unyanyapaa dhidi ya watu walioathirika na ugonjwa huo.
Akizungumzia kuendelea kupungua kwa misaada ya wafadhili kwa shughuli za UKIMWI Dk. Shein ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutafuta namna bora ya kusaidiana na taasisi kama ZAPHA+ ili kutekeleza majukumu ya mapambano dhidi ya UKIMWI.
Kituo hicho kimejengwa na Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ugonjwa wa UKIMWI Zanzibar ZAPHA+ kwa msaada wa taasisi ya Stephen Lewis Foundation ya Canada ambayo ilichangia shilingi milioni 43.65 ambazo ni sawa na asilimia 40.45
Hata hivyo Dk Shein ametoa wito kwa uongozi wa ZAPHA+ kutafuta njia za kujiongezea mapato kwa kubuni miradi ikiwemo ya kujitegemea.
Amewataka wananchi kutumia fursa ya kuwepo kwa jumuiya hiyo kwa kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu maradhi ya UKIMWI kwa manufaa yao binafsi na pia kama sehemu ya jitihada za pamoja kupambana na maradhi hayo nchini.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamuhuna, Waziri wa Afya Juma Duni Haji,Mkuu wa Mkoa Mjini Maghribi Abdalla Mwinyi Khamis na washirika mbalimbali wanaounga mkono mapambano dhidi ya UKIMWI yakiwemo Mashirika ya Kimataifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni