Habari

Jumamosi, 1 Februari 2014

Chadema tutasusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba ikiwa hoja ya kuundwa kwa Serikali tatu itapingwa na wabunge wa CCM.

                                                    Chadema kususia Bunge la Katiba                                                                                                  Wakati Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema wabunge wa chama chake watasusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba ikiwa hoja ya kuundwa kwa Serikali tatu itapingwa na wabunge wa CCM, Mwakilishi wa Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa Ladhu ametaka kuvunjwa kwa Muungano.                                                                                                        


Akihutubia kwenye Uwanja wa Tubuyu nje kidogo ya Mji wa Morogoro juzi, Mbowe alisema wabunge wa chama chake wataandamana nchi nzima kufikisha ujumbe kwa wananchi kwamba maoni yao yamepingwa na wabunge wa CCM walio wengi.
“Tutawaeleza wananchi kwamba maoni ya CCM ndiyo yameonekana ya maana kuliko ya wananchi ambao ni wengi zaidi,” alisema Mbowe kwenye mkutano huo ambao ni sehemu ya Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko – M4C Pamoja Daima.
Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikusanya maoni na kubaini kuwa asilimia 62 ya Watanzania wanataka Serikali tatu za Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano.
“Serikali ya CCM haitaki kusikia maneno Serikali tatu wanasema sera yao ni ya Serikali mbili, wanafanya kila hila ili kuikataa hoja hiyo. Natangaza kwamba wakifanya hivyo tutasusia na kwenda kuwashtaki kwa wananchi,” alisema Mbowe.
Aliongeza kwamba wataandamana kuanzia Kagera hadi Mtwara kuwaeleza wananchi kwamba hoja yao imepingwa na CCM.
Mbowe alisema baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa kashfa dhidi ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kwamba amechukua maoni ya Chadema.
“Wanakosea hayo si maoni ya Chadema, bali ni maoni ya wananchi, Warioba amezingatia maoni ya wananchi,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema Katiba inayotafutwa si ya chama, bali ni ya Watanzania na kwamba inashangaza CCM kuipinga hoja Serikali tatu.
“Tunafahamu wanaogopa kuikubali hoja ya Serikali tatu kwa sababu wanafahamu huo ndiyo utakuwa mwisho wao wa kuwa madarakani,” alisema Mbowe huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Alisema CCM wanaelewa kwamba kukiwa na Serikali tatu, Chadema kitashinda Tanganyika na CUF Zanzibar katika uchaguzi wowote utakaoitishwa.
“Kwa hiyo hivi sasa wana wasiwasi kweli, wanatafuta kila njia ya kuichakachua hoja ya Serikali tatu lakini wafahamu kuwa Chadema wanaifuatilia hoja hiyo kwa ukaribu,” alisema.
Aliwataka wananchi kufuatilia Bunge Maalumu la Katiba litakapoanza mwezi ujao ili kuangalia wabunge wao wanavyowawalisha katika suala hilo muhimu.
Hata hivyo, Mbowe alisema chama hicho kikishinda katika uchaguzi wa mwaka 2015 hakitahangaika kulipa kisasi kwa kuwachukulia hatua za kisheria viongozi, bali kitajikita kutafuta maendeleo.
“Wasituogope tutasamehe kama alivyosamehe aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Hatutalipa kisasi tukiingia Ikulu, kwa sababu hakuna binadamu asiye na makosa. Tutaelekeza nguvu zetu kuwaletea maendeleo Watanzania,” alisema Mbowe.
Jussa na Muungano
Akihutubia mkutano wa kampeni katika Jimbo la Kiembesamaki jana, Jussa alisema hakutakuwa na maendeleo yatakayofikiwa Zanzibar ikiwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hautang’oka.
Jussa ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la CUF, alisema Zanzibar yenye watu milioni 1.5 haiwezi kuwa na tatizo la watu kukosa ajira lakini sera na mipango ya kiuchumi imekuwa ikikwama katika utekelezaji wake kutokana na kukosa mamlaka kamili.
Alisema Zanzibar haiwezi kukopa katika taasisi za kimataifa bila ya kuwekewa dhamana na Waziri wa Fedha wa Muungano wakati Zanzibar ni nchi na kuwataka wananchi kutumia kura zao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuleta mabadiliko ya kiutawala.
“Hakuna sababu ya vijana Zanzibar kukosa ajira, kuna watu wasiozidi milioni 1.5, Muungano umefika wakati ung’oke, ndiyo kikwazo cha maendeleo ya Zanzibar na watu wake kiuchumi na kisiasa,” alisema Jussa.
Alisema mradi wowote unaobuniwa Zanzibar hauwezi kupata mfadhili bila kuwekewa dhamana na Serikali ya Muungano na kukwama kwa juhudi zote za kujiunga na jumuiya za kimataifa akitolea mfano Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC).
Alisema Rais wa Zanzibar amepoteza mambo muhimu chini ya mfumo wa Muungano ikiwa ni pamoja na kutopigiwa mizinga 21 akiwa nje ya nchi, kupeperusha bendera ya Zanzibar, kutokagua gwaride na kupigiwa wimbo wa Taifa la Zanzibar.
“Haya ya sasa si mamlaka kamili, wapi Dk Shein alikokwenda akapigiwa mizinga 21 au alipeperushwa wapi bendera ya Zanzibar wakati wa safari zake za nje?” alihoji Jussa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni