Habari

Jumatano, 2 Oktoba 2013

MCT yazindua shindano tuzo mwandishi 2013

NA RICHARD MAKORE


Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tuzo za EJAT, Kajubi Mukajanga
Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na wadau limetangaza shindano la kumtafuta mwandishi mahiri wa tuzo za EJAT kwa mwaka 2013.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tuzo hizo, Kajubi Mukajanga, alitangaza hayo jana ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema shindano hilo hufanyika kila mwaka na linalenga kuwapa hamasa waandishi wa habari nchini kuibua na kuandika vitu vinavyoisaidia jamii.

Alitaja maeneo yatakayoshindaniwa kupitia shindano hilo kuwa ni pamoja na kuangalia habari nzuri zilizoandikwa mwaka 2013,  kuhusu uchumi na biashara, michezo na utamaduni, mazingira, afya, HIV/AIDS, watoto, utawala bora, jinsia, sayansi na teknolojia, malaria, uchunguzi na elimu.

Maeneo mengine yatakayoshindaniwa kupitia shindano hilo ni habari nzuri zilizoandikwa mwaka 2013, kuhusu, utalii, walemavu, mpigapicha bora wa magazeti, mpigapicha bora wa televisheni, mchora katuni bora, kilimo na biashara ya kilimo, afya ya uzazi na kundi maalumu la wazi.

Alisema hii ni mara ya tano wanaandaa shindano hilo na kwamba, mara ya kwanza, walianza mwaka 2009.
Kwa mujibu wa Mukajanga, moja ya vigezo wanavyoangalia, ni pamoja na habari husika namna ilivyoisaidia jamii na nguvu za ziada zilizotumiwa na mwandishi kuitafuta na kuiandika.

Wakati EJAT, ambao ni waandaaji wa shindano hilo wakitangaza kuanza kupokea kazi za waandishi zilizofanyika mwaka 2013 ili kuzishindanisha, mashindano ya mwaka 2012 yalizua malalamiko miongoni mwa washiriki.
 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni