Mfumo huo ambao unatarajiwa kuanza kutumika kwenye Mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka huu, unakuja ikiwa ni miezi michache tangu Tume ya Waziri Mkuu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha kufeli kwa maelfu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012.
Akizungumzia mchakato huo, Kamishna wa Elimu Profesa Eustella Bhalalusesa alisema kwamba hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni sehemu ya kuboresha elimu na kuwa haina uhusiano na taarifa ya tume iliyoundwa na Waziri Mkuu ambayo mpaka sasa haijawekwa hadharani.
“Mambo yanakwenda yanabadilika hata binadamu yeyote anabadilika kila siku, mfumo unaotumika sasa hivi ni wa siku nyingi,” alisema.
Alisema kuwa, ili kuweza kuboresha vyema mfumo huo wameshirikisha wadau mbalimbali zikiwamo shule za sekondari.
“Kama unataka kuboresha lazima upate maoni, lengo letu ni kushirikisha shule zote za sekondari za Tanzania, ila siwezi kukuhakikishia kama zote zitashiriki kwa kuwa tunawatumia zaidi maofisa elimu mkoa na wilaya. Tumeweka pia dodoso kwenye mdandao ili watu zaidi washiriki.
Kuhusu tume ya Pinda hapa haihusiki kabisa, ile ilikuwa na mambo yake, hata bila ile tume sisi hii tungefanya tu,” alisema Profesa Bhalalusesa.
Alisema kuwa, mpaka sasa wameshapokea zaidi ya asilimia 60 ya maoni hayo kutokana na lengo walilo jiwekea.
Dodoso hilo ambalo pia Mwananchi imefanikiwa kuliona, linasema kuwa serikali inakusanya maoni ya wadau wa elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na cha sita pamoja na matumizi ya ‘Alama Endelevu ya Mwanafunzi [Continuous Assessment (CA)].
“Serikali imeamua kukusanya maoni haya kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na kidato cha sita havifanani pamoja na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari.
Pia mfumo wa elimu ya sekondari umekuwa na miundo tofauti ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta),” sehemu ya dodoso inasema.
CHANZO- MWANANCHI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni