Wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akisisitiza kuwa hesabu za Chadema ni miongoni mwa ambazo hazijakaguliwa, chama hicho kimeishutumu kamati hiyo kwa kuagiza kusitishwa kwa ruzuku kwa vyama vya siasa na kusema hatua hiyo ni ubabe.
Wakati Chadema wakitoa kauli hiyo, jana Zitto alisema vyama vya siasa tisa vikiwamo Chadema, CCM na CUF vinatakiwa kufika mbele ya PAC Oktoba 25 mwaka huu, kwa ajili ya kujieleza na kwamba chama kitakachokaidi, sheria za Bunge zinaeleza wazi, kwamba wahusika wanaweza kufungwa jela siku saba.
Chadema kilisema kuwa PAC kabla ya kuchukua hatua, ilipaswa kuwapa nafasi ya kuwasikiliza viongozi wa vyama husika, kumhoji Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Msajili wa vyama vya Siasa ambao wameshindwa kutimiza wajibu wa kukagua hesabu hizo kwa miaka minne.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu alisema jana kuwa, uamuzi wa PAC utaviathiri vyama kwani bajeti zake zimezingatia kuwapo kwa ruzuku.
“Kuna vyama ambavyo vinategemea ruzuku kulipa mishahara ya wafanyakazi wake, Chadema ingawa tuna vyanzo vingine vya mapato, tunaitegemea kukamilisha bajeti yetu kwa fedha za ruzuku ambazo zinatusaidia kwa asilimia 45. Ni tabia mbaya kuchukua uamuzi kwa kibabe na kuhukumu kabla ya kutusikiliza siyo haki hata kidogo,” alisema Komu.
Alitetea chama chake kwamba kimekuwa na utaratibu wa kuwasilisha hesabu zilizokaguliwa ambapo alitoa ushahidi wa barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya April 16, 2012 ikithibitisha kwamba hesabu zao zipo sawa baada ya kuziwasilisha katika ofisi hiyo.
“Chadema tunataka ukaguzi wa hesabu usijikite katika fedha za ruzuku pekee bali katika vyanzo vyote vya mapato ya vyama, tatizo CAG alitueleza kwamba anakabiliwa na upungufu wa rasilimali watu kwa hiyo PAC walipaswa kuliangalia tatizo hilo na kutafuta ufumbuzi,” alisema Komu.
Zitto juzi alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa Serikali ilitoa kiasi cha Sh67.7 bilioni kama ruzuku kwa vyama tisa vya siasa tangu mwaka 2009, lakini vyama hivyo havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu zake kwa msajili kama sheria inavyoagiza.
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema), aliamuru Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kusimamisha utoaji wa ruzuku hadi hapo vitakapowasilisha ripoti ya ukaguzi na makatibu wake wakuu kuhojiwa.
Miongoni mwa vyama vilivyotajwa ni APPT-Maendeleo lakini jana Rais Mtendaji wa Chama hicho, Peter Mziray alisema chama chake hakijawahi kupewa kiasi cha Sh217 milioni kama inavyodaiwa na PAC.
Mziray alikiri walianza kupata ruzuku 2009 ila inasema ilikuwa kidogo kiasi cha Sh 50,000 kwa mwezi na baadae kupanda Sh 275,000 kwa mwezi.
Alisema kiasi walichopata kuanzia mwaka 2009 ni kiasi cha Sh12 milioni tu. “APPT-Maendeleo haina uwakilishi bungeni kwa hiyo haiwezi kupata kiasi hicho kikubwa cha fedha,” alisema Mziray.
CHANZO- MWANANCHI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni