Habari

Jumatatu, 14 Oktoba 2013

Patashika Ikulu leo

•  JK KUJADILI MUSWADA NA MBOWE, LIPUMBA, MBATIA
JUMANNE OKTOBA 15,2013.
na Mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete leo anakutana Ikulu na viongozi wa vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kwa ajili ya mazungumzo ya kuboresha kasoro zilizojitokeza kwenye muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.
Hatua hiyo inatokana na msimamo wa wabunge wa vyama hivyo kususia mjadala wa muswada huo uliopitishwa hivi karibuni na wabunge wachache wa CCM na Augustine Mrema wa TLP, wakidai umechakachuliwa, huku Zanzibar ikiwa haijashirikishwa.
Kufuatia kusigana huko, viongozi wa vyama hivyo; Freeman Mbowe (CHADEMA), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), walikutana na makundi mbalimbali ya wadau na kutangaza kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kupinga rais asisaini muswada huo.
Uamuzi wa wapinzani hao uliwaibua mawaziri kadhaa, Stephen Wassira (Ofisi ya Rais-Mahusiano na Uratibu), William Lukuvi (Sera, Uratibu na Bunge), Mathias Chikawe (Katiba na Sheria) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema wakiwabeza.
Mawaziri hao walidai wapinzani wanapoteza muda wa mchakato ili rais awaite Ikulu tena kwa mazungumzo waweze kunywa chai na juisi, jambo walilosisitiza kuwa haliwezekani, kwani milango hiyo imefungwa.
Hata Waziri Chikawe alifikia hatua ya kumtisha Rais Kikwete, akisema kuwa asipousaini muswada huo atakuwa ametangaza mgogoro na Bunge, kwani lilifanya kazi yake kwa kufuata Katiba.
Rais Kikwete alitilia maanani hoja za pande zote na kuamua kuwaita wapinzani mezani kuzungumza nao, akisema kuwa kama dhamira yao ni kutaka kupata Katiba mpya, anawashauri waachane na mipango ya maandamano na kufanya ghasia, bali watumie njia halali, kwamba serikali iko tayari kuwasikiliza.
Hoja zinazovutaniwa
Mbali na mambo mengine, wapinzani wanadai kuwa muswada huo ulichomekwa baadhi ya vipengele ambavyo vingeisaidia CCM kutawala mchakato mzima wa katiba.
Katika hoja ya mapendekezo ya kumpa rais mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu, wapinzani hao wanasema hayakubaliki, kwamba yanarudisha dhana kwamba wajumbe hawa watakuwa watu wa rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.
“Sheria iweke wazi kwamba wajumbe hawa ‘watateuliwa’ na taasisi zilizotajwa. Hii itaondoa utata juu ya uwakilishi wao na juu ya mamlaka yao ya uteuzi.
“Sheria itaje kwamba idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu watakaotokana na kila taasisi iliyoorodheshwa katika kifungu cha 22(1)(c) itakuwa 354,” walisema wapinzani.
Katika suala la Zanzibar, wapinzani hao wanasema wananchi wa huko hawakushirikishwa wakati wa uandaaji wa muswada huo, hivyo kutaka mambo kadhaa yafanyike ili kuondoa mgongano.
Kwamba, ili kutimiza matakwa haya ya sheria na kwa kuzingatia mapendekezo ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume, Bunge linahitaji kuangalia upya suala la uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalumu.
Kwa mujibu wa kifungu cha 22(2) cha Sheria, idadi ya wajumbe wa Zanzibar katika Bunge Maalumu watakaotokana na makundi yaliyoainishwa katika kifungu cha 22(1)(c) “... haitapungua theluthi moja ya wajumbe hao.”
Hii ina maana kwamba, kwa uchache kabisa, wajumbe hao wa Zanzibar hawatapungua 55.
Rasimu ya Katiba itakayojadiliwa na Bunge Maalumu inahusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano peke yake. Rasimu hiyo imependekeza kwamba masuala yote yasiyo ya Muungano, ya washirika wa Muungano, yaani Tanzania Bara na Zanzibar, yashughulikiwe na Katiba za washirika hao.
Rais Kikwete katika kutambua hoja za wapinzani aliomba hekima ziwaongoze viongozi wa pande zote ili waweze kutumia utaratibu walioutumia mwaka 2012.
“Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo,” alisema rais.
Aliongeza kuwa kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu na kutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa hawatengenezi katiba ya chama fulani bali katiba ya nchi, katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndio wengi kuliko wote.
Kuhusu ushiriki wa Zanzibar, alisema kuwa alielezwa ni kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilivyoshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika muswada.
“Kama ni hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe bungeni ili wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulaumiana isivyostahili,” alisema.
Suala la Tume ya Mabadiliko ya Katiba nalo litakuwa sehemu ya mjadala huo, licha ya Rais Kikwete naye kuona umuhimu wake akitaka ihusike kwenye hatua ya Bunge Maalumu.
“Nimeulizia ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na pendekezo la mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na wabunge wengi.
“Nami naiona hoja ya wajumbe wa tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalumu, hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya tume,” alisema.

CHANZO-TANZANIA DAIMA.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni