Habari

Ijumaa, 4 Oktoba 2013

Wahamiaji kadhaa wa Kiafrika wafa, wapotea katika ajali ya boti pwani ya Italia




  • Kiasi cha watu 92 walikufa maji na wengine 200 wanaaminiwa kupotea baada ya boti iliyokuwa na watu 500 wanaoomba hifadhi kutoka Afrika kushika moto na kuzama karibu na upwa wa Italia siku ya Alhamisi (tarehe 3 Oktoba), walisema maafisa wa serikali.
"Tuna maiti 92 na watu 151 wameokolewa. Tunawatafuta watu wengine walio hai majini," msemaji wa walinzi wa pwani aliliambia shirika la habari la AFP, akiongeza kwamba msako ulikuwa ukiendelea kwa zaidi ya masaa sita.
Watafutaji hao hifadhi walisema walikuwa wanatokea Eritrea na Somalia, na polisi wa eneo hilo walinukuliwa wakisema waliamini kuwa boti hiyo ilitokea pwani ya Libya.
Giusi Nicolini, meya wa kisiwa cha Lampedusa kilicho karibu na ajali ilikotokea, alisema wahamiaji hao waliwakuwa wamemwambia kwamba waliwasha moto kwenye kwenye boti hiyo umbali wa maili moja kutoka ufukwe ili kuwaita walinzi wa pwani baada ya chombo chao kupata matatizo ya injini.
Moto huo baadaye ulisambaa, ukasababisha hofu ndani ya boti ambako kulipelekea boti hiyo kuelemea upande mmoja na kuzama.
"Manusura wako katika hali ya mshtuko," alikiambia kituo cha habari cha Sky TG24. "Wamekuwa majini tangu nyakati za alfajiri."
Huku matumaini ya kuwapata manusura zaidi yakipungua, walinzi wa pwani, wapiga doria ya mipakani, kikosi cha zimamoto na jeshi la majini wote walikuwa wakishiriki kwenye msako na waliungana na boti za wavuvi na za kifahari.
"Huu ni msiba bila ya shaka yoyote. Katika miaka yangu mingi ya kazi hapa, sijawahi kuona kitu kama hiki," Pierto Bartolo ambaye ni daktari kwenye eneo hilo alinukuliwa akisema hivyo na shirika la habari la Italia, ANSA. "Hatuhitaji magari ya kubebea wagonhwa, kwa bahati mbaya, tunahitaji magari ya kubebea maiti. Bado kuna mamia waliopotea."
Miili ilikuwa ikipelekwa kwenye ghala la uwanja wa ndege wa eneo hilo kwa sababu hakukuwa na nafasi tena kwenye jengo la kuhifadhia maiti kwenye kisiwa hicho cha mbali kusini mwa Italia, ambacho kina idadi ya wakaazi wapatao 6,000.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni