Katika hali isiyo ya kawaida kijana mmoja anayetambulika kwa jina la Alhaji maarufu kwa jina la Okwi, ametoroka kwao Kigoma kuja Dar es Salaam kwa usafiri wa kuungaunga ili amwone straika huyo wa Uganda.
Kijana huyo alifikia Kariakoo, Dar es Salaam na hana ndugu wala mtu anayemfahamu hivyo akawa anaganga mchana na usiku analala nje kwenye mabanda ingawa kwa sasa amepata msamaria mwema anayetambulika kwa jina la Salim Simba. Msamaria huyo amemchukua na anaishi naye nyumbani kwake Buguruni, Dar es Salaam.
Kijana huyo ambaye pia ni shabiki wa Simba, amekuwa akiambatana na wachezaji pamoja na viongozi wa Simba na katika siku za karibuni hakosekani uwanjani kwenye kidedea cha Simba akiishangilia timu hiyo.
Ili kukata kiu yake, wakati wote huu ambao Okwi yuko jijini Dar es Salaam, kijana huyo huketi sambamba na Mganda huyo katika mechi ambazo Okwi hufika uwanjani kuishuhudia Simba.
Alhaji ambaye pia huwa hakosi kwenye mazoezi ya Simba alizungumza na Mwanaspoti: “Nilitoka kwetu Kigoma kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kumwona Okwi, lakini ilikuwa bahati mbaya ndiyo akawa ameondoka. Nilikuja kiujanja ujanja hadi nikafika hapa. Sikuwa na ndugu ninayemfahamu kwa hiyo nikawa nakaa Kariakoo nje ya jengo la klabu, nazunguka na jua linapozama nalala nje.”
Akimzungumzia kijana huyo, Simba ambaye anakaa naye kwa miezi miwili sasa alisema: “Kama shabiki wa Simba niliona huruma kitendo cha yeye kulala nje kwenye mabanda ambako hakuna ulinzi wa aina yoyote na nikifikiria ujio wake Dar es Salaam ni kwa ajili ya Okwi ndiyo nikaona nimchue.
“Nilimuuliza kuhusu wazazi wake na kumwambia anipe namba zao za simu niwasiliane naye, lakini namba zote alizonipa hazipatikani, sasa sina cha kufanya nimeamua kujitolea tu.” Juhudi za kumtafuta Okwi ili kujua uamuzi wake juu ya kijana huyo hazikufanikiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni