Na Haji Nassor, Pemba.
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kujenga kituo cha mawasiliano kwa njia ya picha (video conference) katika Ikulu ya Zanzibar , wakati wowote kuanzia sasa, ili kurahisisha mawasiliano kwa njia ya picha.
Vituo hivyo kwa Zanzibar vitajengwa vinne, ikiwemo ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na chengine kinatarajiwa kujengwa kisiwani Pemba .
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa njia ya mawasiliano ya picha (microwave link) Michakani Chake Chake Pemba , Waziri wa Sayansi na Teknolojia, ProF.Makame Mnyaa Mbarawa, alisema mradi huo uko katika hatua za mwisho.
Alisema tayari mradi huo umeshaunganishwa mikoa yote ya Tanzania Bara, ambapo miongoni mwa faida hizo ni kuonana na mtu mnaewasiliana.
Alisema mradi huo utaharakisha mawasiliano hasa kwa njia ya picha ambapo wazungumzaji wataweza kuwasiliana moja kwa moja.
Alisema njia hiyo ya mawasiliano kama ikitumiwa vyema, inaweza kuwa chachu ya kuinua uchumi na kukuza kiwango cha mawasilino nchini.
"Njia hii ya mawasiliano ndio chachu ya kufikia mafanikio ya kiuchumi, kisiasa kijamii na kiutamaduni, kutokana na kuibua mambo mengi ya kujifunza kwa mtumiaji,” alisema.
Katika hatua nyengine Waziri huyo alikemea vikali baadhi ya wananchi wenye tabia ya kuharibu miundombinu ya mamwasiliano, ambapo tabia hiyo inaweza kuirejesha nyuma Tanzania kiwamawasiliano.
Alisema amekuwa akisikia kupitia vyombo vya habari kuwepo kwa baadhi ya watu kisiwani Pemba wenye tabi hiyo, jambo ambalo limemshitua sana .
"Wenzetu wa kampuni ya simu ya TTCL tayari wametuonyesha njia kuelekea kwenye mafanikio ya kitaalamu, kazi kubwa ilioko mbele yetu ni kuwaunga mkono,” alisema.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Tanzania, Peter Ngota, alisema mradi huo uliozinduliwa jana, ulianza kazi zake rasm Disemba 2012 na kumalizika mwishoni mwa mwaka jana.
Alisema mradi huo wa TEHAMA ambao umefadhiliwa na serikali ya Japan kwa gharama ya dola za kimarekani 1.589 milioni, umeongeza uwezo wa ujazo wa mawasiliano kutoka 32 hadi 155 kwa sasa.
Nae Mjumbe wa bodi ya kampuni ya TTCL,Sheha Mohamed Sheha, alisema kwa muda mrefu kampuni hiyo ilikuwa imedorora ingawa kwa sasa imeamka na inakabiliana na ushindani wa kibiashara.
Nae Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, Mhe. Rashid Seif Suleiman, aliipongeza serikali ya Japan kutokana na misaada yake ukiwemo mradi huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni