Habari

Jumamosi, 26 Aprili 2014

MAALIM SEIF; SIKUMMALIZA JUMBE.


Mwaka 1984, Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na Makamo wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aboud Jumbe Mwinyi, alilazimishwa kujiuzulu katika Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma akishutumiwa kutaka kuvunja Muungano. Kitendo hiki kimekuwa kikichukuliwa na Wazanzibari kama udhalilishaji mkubwa kwa nchi na heshima yao, na msimamo wa serikali tatu, ambao Jumbe anasemekana kuutetea umekuwa ndio msimamo wa Wazanzibari. Kujiuzulu kwa Jumbe kunaunganishwa na tafauti za kimtazamo baina yake na Katibu Mkuu wa sasa wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye hata hivyo anasisitiza katika makala hii kwamba hajawahi kutafautiana na Jumbe kuhusu mtazamo wa Muungano.
Kwanza niweke kumbukumbu sawa. Mwaka 1984 wakati Mzee Aboud Jumbe anajiuzulu nyadhifa zake zote, mimi ni kweli nilikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, na hivyo kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi. Hata hivyo wakati huo sikuwa miongoni mwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi. Kwani nilikuwa Waziri wa Elimu wa Zanzibar kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1980. Nikateuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar na Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyeteuliwa kuwa Rais wa Muda wa Zanzibar mara baada ya Mzee Aboud Jumbe kujiuzulu mwaka 1984. Hivyo kuanzia mwishoni mwa 1980 hadi mwanzoni mwa 1984 sikuwa kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi.
Pili, tangu Chama cha Wananchi CUF kiasisiwe hapo 1992, sera yake rasmi ni kuwepo kwa Muungano wa serikali tatu: yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika.
Pengine itakumbukwa kuwa hata Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kuwa Chama cha Siasa chochote kile kina haki ya kuwa na sera yake juu ya Muungano. Akasema kuwa kama vile ni haki ya CCM kuwa na sera ya serikali mbili kuelekea serikali moja, CUF wanayo haki hiyo hiyo ya kuwa na sera ya serikali tatu katika Muungano. Mwalimu Nyerere akamalizia kwa kusema kuwa na sera juu Muungano inayotafautiana na sera ya CCM si uhaini. Waachiwe wananchi waamue!
Hivyo basi msimamo wangu tangu kuasisiwa kwa Chama cha Wananchi, CUF haujapata kubadilika. Ni msimamo na sera ya Chama changu cha CUF. Sera ya kuwepo kwa serikali tatu katika Muungano wetu.
Hivyo niseme, kama nilivyokuwa nikisema kila nilipopata nafasi, kuwa bila ya kuubadili muundo wa Muungano wetu kutoka muundo wa sasa wa serikali mbili kwenda kwenye muundo wa serikali tatu, matatizo ya Muungano yataendelea kuutafuna Muungano wetu. Badala ya kuuimarisha tutakuwa tunaendelea kuudhoofisha. Kuimarisha Muungano sio kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano katika Katiba. Hili linadhoofisha Muungano. Kwani nguvu za Muungano zitatokana na wananchi wa pande mbili kuukubali kwa dhati Muungano wenyewe. Kuhakikisha kuwa wananchi wa pande zote mbili wanaridhika na muundo wake, mamlaka na madaraka ya kila upande na serikali yake. Na zaidi kuliko yote, wananchi wa pande zote mbili kuridhika kuwa wanatendewa haki katika Muungano.
Vyenginevyo tutakuwa tukibadili misamiati tu: mara tutayaita matatizo ya Muungano; mara tuziite kero za Muungano, pengine tutakuja kuyaita mapungufu ya Muungano, au hata bughdha za Muungano, na kadhalika.
Suala la kutoka serikali mbili kwenda serikali moja hilo halitakubalika. Mimi silikubali. CUF hailikubali, na Mzanzibari mzalendo yeyote halikubali. Siamini kuwa Serikali ya Muungano itakuwa tayari kutumia vifaru, mizinga na madege ya kivita kulazimisha muundo wa serikali moja.
Baada ya kuweka msimamo huo, sasa nigeukie mambo mengine uliyoniuliza.
Kwamba Mzee Aboud Jumbe alituhumiwa kutaka kuwepo kwa muundo wa Muungano wa serikali tatu na akalazimishwa kujiuzulu. Wakati huo mimi nilitetea muundo wa sasa wa serikali mbili.
Ili hili lifahamike vyema na wananchi ni vyema kwanza kuelezea mazingira yaliyomfikisha Mzee Aboud Jumbe kujiuzulu.
Nitangulie kueleza kuwa mimi binafsi na kwa dhati ya nafsi yangu namuheshimu na namthamini sana Mzee Aboud Jumbe. Kwanza ni mwalimu wangu nilipokuwa nasoma katika skuli ambayo wakati huo ikiitwa The King George VI Secondary School (sasa Lumumba College).
Pili, ni Mzee Aboud Jumbe ambaye alisababisha mimi kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara baada ya yeye kuwa Rais wa Zanzibar mwaka 1972, baada ya kukaa kwa miaka minane (8) tangu nilipomaliza masomo ya Kidatu cha Sita (Form VI) hapo 1963 na kuzuiwa na Serikali ya Mapinduzi kujiunga na masomo ya Chuo Kikuu, pamoja na kuwa kila mwaka nilikuwa napata nafasi katika vyuo mbali mbali duniani.
Tatu ni Mzee Aboud Jumbe huyo huyo aliyesababisha mimi kuwa kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi na kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa CCM. Hivyo namshukuru na katu siwezi kumsahau kwa mchango wake mkubwa ulionifanya nilivyo.
Sasa nirejee kuelezea mazingira ya wakati huo ambayo yalikuwa kama ifuatavyo:
Nianzie mwaka 1982 ambapo kulikuwa na uchaguzi wa viongozi wa CCM. Katika kipindi kilichotangulia Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM wa 1982 wa kuchagua viongozi wa kitaifa, kulijitokeza makundi mawili miongoni mwa viongozi wa CCM kutoka Zanzibar yaliyokuwa yakikinzana. Kundi la kwanza likijulikana kama Liberators, na la pili likijulikana kama Frontliners. Kundi la Liberators kimsingi lilikuwa na viongozi ambao walikuwa wanapinga mabadiliko ya aina yoyote yale katika uendeshaji wa mambo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Zanzibar.
Kwa lugha ya sasa unaweza ukaliita kundi la Wahafidhina. Kundi la Frontliners lilikuwa na vijana, damu mpya iliyoingia katika uongozi wa Chama na SMZ. Kundi hili lilitaka mabadiliko katika uendeshaji wa mambo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Unaweza ukaliita kundi la Reformers.
Uchaguzi wa viongozi wa kitaifa (Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa) wa 1982 ulishuhudia msuguano mkali kati ya makundi hayo mawili. Nia ya Liberators ilikuwa ni kuhakikisha kuwa Frontliners hawaingii katika Halmashauri Kuu ya Taifa. Nia ya Frontliners ilikuwa ni kuhakikisha damu mpya inaingia katika kikao hicho kikuu cha maamuzi cha Chama ambacho wakati huo kilikuwa ndio kimeshika hatamu zote za uongozi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bahati njema Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, kwa busara zake, uliwaingiza watu kutoka makundi yote mawili katika NEC na, baadaye, NEC ikawaingiza watu kutoka makundi yote mawili katika Kamati Kuu.. Frontliners walishukuru kuona kuwa miongoni mwao walifanikiwa kuchaguliwa kuingia katika vikao vyote viwili vikuu vya maamuzi vya Chama.
Kwa upande mwengine, Liberators hawakufurahi. Liberators hao walishaweka shinikizo kwa Mzee Aboud Jumbe (ambaye ndiye chanzo cha kuingiza damu mpya katika CCM ya wakati huo) kuwa vijana aliowaingiza watakujamgeukia na kuwaondoa wao, Liberators, na yeye mwenyewe katika uongozi. Inaelekea Mzee Aboud Jumbe alishawishika na shinikizo hilo, na hivyo naye, kwa njia zake (nyuma ya pazia), alitaka kuona kuwa Frontliners hawaingii katika NEC na Kamati Kuu ya Chama ambako pengine wangekuwa na ushawishi katika maamuzi ya sera za Chama. Frontliners walipoingia, ikawalazimu Liberators na Mzee Aboud Jumbe kutafuta njia nyengine ya kuweza kuwazingira ili, ikiwezekana, waweze kuondolewa katika ramani ya uongozi wa Chama na Serikali.
Hivyo basi, mara baada ya kikao cha Mkutano Mkuu wa Taifa kumalizika mwezi Novemba, 1982, Mzee Aboud Jumbe aliwataka Wajumbe wote wa NEC kutoka Unguja akutane nao Unguja, na Wajumbe wote wa NEC kutoka Pemba akutane nao Pemba. Katika mikutano hiyo, hotuba ya mwalimu wangu, Mzee Aboud Jumbe, ilitushtua wengi. Mzee Aboud Jumbe alishtumu kuwa kuna watu wanaoleta uchochezi kutaka kuvigawa visiwa vya Unguja na Pemba; kutaka kuigawa mikoa, yaani mkoa mmoja dhidi ya mwengine katika kila kisiwa; kutaka kuzigawa wilaya, yaani wilaya moja dhidi ya nyengine katika kila mkoa; na kutaka kuvigawa vijiji, yaani kijiji kimoja dhidi ya chengine katika kila wilaya. Akamalizia kwa kusema kuwa watu hao watahukumiwa na kuonja kile alichokiita “Revolutionary Justice”
Hili lilitushtua wengi, hasa sisi vijana wa wakati huo. Tukakumbuka historia ya Zanzibar tangu Mapinduzi ambapo watu walioshukiwa kuwa wapinzani wa serikali, na hasa wasomi, walivyoshughulikiwa kwa kuhakikisha kuwa wanatoweka kabisa. Khofu yetu ikawa jee, hawa wazee si wamekusudia kuturudisha huko huko tulikotoka? Tukasema kama hatukuchukua hatua za kichama kulizuia hili, basi kuna uwezekano wa historia kujirudia na watu wasiokuwa na hatia kupotea kwa kile kinachodaiwa kusimamisha “Revolutionary Justice”
Hivyo baadhi yetu tuliokuwa Wajumbe wa Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama, hasa sisi kutoka Zanzibar, tukamfuata Mzee Rashid Kawawa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM na Mwenyekiti wa Sekretarieti na kumueleza khofu yetu hiyo. Mzee Kawawa akatuelewa na akaamua iletwe agenda juu ya suala hilo katika kikao kilichofuata katika Sekretarieti. Agenda ikaletwa. Ikajadiliwa kwa mapana yake, kisha ikawasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu. Kamati Kuu ikaamua kuunda timu mbili kwenda kuchunguza madai yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Aboud Jumbe. Timu moja ikaagizwa kufanya uchunguzi katika kisiwa cha Unguja, na timu ya pili ikaagizwa kufanya uchunguzi katika kisiwa cha Pemba. Timu moja iliongozwa na Marehemu Moses Nnauye na ya pili iliongozwa na Mheshimiwa Alfred Tandau.
Baada ya uchunguzi, timu zote mbili zikawasilisha taarifa zao katika kikao cha Kamati Kuu. Timu zote mbili ziliona kuwa madai ya Mzee Aboud Jumbe hayakuwa na msingi. Hivyo Kamati Kuu ikamsihi Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Makamu wa Mwenyekiti wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Aboud Jumbe, kuzuia kuchukua hatua zozote zile ambazo zingeweza kusababisha ukiukwaji na uvunjaji wa haki za binadamu dhidi ya raia.
Inavyoonekana, hili halikumpendeza mwalimu wangu, Mzee Aboud Jumbe. Alihisi kuwa Chama, na Muungano unamuingilia katika kutekeleza azma yake na ile ya Liberators ya kuisafisha safu ya uongozi wa Chama Zanzibar kwa kuwaondoa kwa njia yo yote ile Frontliners na vijana wenye mawazo mapya .
Kipindi hicho kulikuwa na mjadala ulioanzishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa juu ya mapendekezo ya marekebisho ya Katiba. Mzee Aboud Jumbe na timu yake wakaona kuwa waitumie nafasi hiyo kufanya kampeni kabambe kutaka muundo wa Muungano ubadilishwe. Sisi wa Frontliners tulitafsiri kuwa kampeni hiyo madhumuni yake ni kutaka kubadili muundo wa Muungano ili kundi la Liberators lipate uhuru zaidi, nguvu zaidi, na madaraka zaidi, ambayo, kwa mawazo yetu, yangetumika dhidi ya watu wenye mawazo mapya na ambao walionekana kama ni tishio kwa Liberators. Tulitafsiri kampeni hiyo kuwa na agenda iliyojificha ya kutaka kujiimarisha na kujichimbia katika madaraka kundi la Liberators ili kulinda “status quo.”
Ni kwa msingi huo ndipo mimi na wenzangu wa Frontliners tulimpinga Mzee Aboud Jumbe. Ifahamike kuwa hatukupinga dhana ya serikali tatu! Tulipinga nia iliyojificha ya Mzee Aboud Jumbe na wenzake ya kuibua agenda hiyo. Tulipinga njia zilizotumika katika kuisimamia na kuiendesha agenda hiyo. Ndio maana mara baada ya Chama cha Wananchi, CUF, kuundwa, tukabuni sera ya muundo wa Muungano wa serikali tatu. Ikumbukwe kuwa wengi wa waasisi wa CUF walitokana na kundi la Frontliners.
Ingalikuwa kulikuwa na nia njema, Mzee Aboud Jumbe angetuita, walau baadhi yetu na kutaka mawazo yetu. Nina hakika wengi tungekubaliana naye na tungezungumzia mkakati wa kulikabili suala hilo. Mimi nina hakika tungekwenda Kamati Kuu na baadaye Halmashauri Kuu kama uongozi wa Zanzibar ulioungana, wenzetu wa Bara wasingeweza kutupuuza. Na hapa niseme, tena kwa masikitiko makubwa, kwamba hili ndio limekuwa tatizo letu Wazanzibari. Wazanzibari tuna madai ya msingi katika Muungano. Lakini tunashindwa kuyasimamia madai yetu hayo hadi kupatikana mafanikio kwa kuwa tumekubali kugawiwa na tumegawika. Kugawika huko hakuyanufaishi maslahi ya Zanzibar.
Nitoe wito, kupitia gazeti lenu, kwamba wakati umefika kwa Wazanzibari bila kujali tafauti zetu za kiitikadi, kuungana ili kusimamia, kutetea na kuendeleza masilahi ya Zanzibar na watu wake katika Muungano.
Kwa kumalizia basi, kwa maoni yangu, Zanzibar ni nchi. Zanzibar ni taifa. Zanzibar ni dola.
Zanzibar ni nchi kwa sababu ni eneo lenye mipaka inayotambulikana na Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia ina watu wanaotambulika.
Zanzibar ni taifa kwa vile Wazanzibari kwa ujumla wao wanatambulikana kuwa na mila na utamaduni wao. Wazanzibari wanaweza kutafautishwa na watu wa sehemu yoyote nyengine duniani. Taifa la Wazanzibari lina uhai na ni taifa endelevu.
Zanzibar ni dola kwa vile kuna mamlaka iliyowekwa na Katiba zote mbili, yaani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye madaraka yasiyoweza kuingiliwa na chombo chochote chengine katika mambo yasiyo kuwa ya Muungano katika nchi ya Zanzibar. Ni kweli kuwa Zanzibar haina jeshi lake wala polisi yake. Lakini ni kweli pia kuwa Zanzibar ina vyombo vyake vyengine vya maguvu vilivyoanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Katiba inayotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano na sheria za Zanzibar. Hivyo ni vyombo vya maguvu vilivyo halali kwa mujibu wa sheria za nchi.
Ni kweli kuwa suala la Mambo ya Nje ni jambo lililomo katika orodha ya Mambo ya Muungano. Lakini ni kweli pia kuwa suala la mahusiano ya kimataifa halijawahi kuingizwa katika orodha ya Mambo ya Muungano. Hivyo Zanzibar ina uwezo kamili wa kushirikiana na mataifa na mashirika ya kimataifa katika kuwaletea maendeleo Wazanzibari. Ni bahati mbaya kuwa Serikali ya Muungano imejaribu na inaendelea kuiminya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusimamia ushirikiano wa kimataifa. Mambo kama haya ndio yanaoudhoofisha Muungano wetu.
Kama kuna watu wanasema kuwa Zanzibar sio nchi, basi wasiishie hapo. Waeleze jee Zanzibar ni Mkoa, au ni Wilaya, au ni kijiji au ni kitongoji?
Chanzo:Mzalendo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni