Na Is-haka
Mohammed,Pemba.
Wananchi kisiwani Pemba wametakiwa kuendelea
kuchukua tahadhari ya kujikinga na Maambukizi ya homa ya Dengue ambayo tayari
baadhi ya kesi za kupatikana wagonjwa wa homa ya dengue faver zimesharipotiwa
kisiwani Unguja.
Akizungumza
katika siku ya afya ya mtoto wa Madrasa huko katika Mtambile, Afisa Lishe
Wilaya ya Mkoani Dk Mwajine Khamis Mjaka amesema kuwa licha ya kutokuwepo na
mtu aliyepata kutambulika na homa ya Dengue wananchi wanapaswa kujiepesha na
hatari ya kuambukizwa homa hiyo inayoenezwa na mbu.
Amesema
kutokana na mbu ndiyo wanaosambaza homa na kuwepo mazingira hatarishi katika
maeneo wanayoishi jamii,upo uwezekano wa kuwepo kwa maambukizi hayo endapo
tahadhari za kujikinga hazitachukuliwa na mapema.
Dk Mwajine
amewataka wananchi kisiwani Pemba kuchukuwa hatua za kujikinga kwa kufukia
madimbwi ili mbu wasizaliane, kutia wavua katika majumba,kutumia vyandarau hata
kwa wale wanaolala mchana.
Aidha
amesema kuwa hatua nyengine za kujikinga ni kuvaa nguo refu na dalili zake ni
mwili kuwa mchovu katika viungo,pia kutoka damu katika sehemu za wazi kama vile
puani na masikio,hivyo kuwataka wananchi wanapoona dalili hizo kukimbilia
hospitali kupata kinga.
Akizungumza
na Zenj FM juu ya siku ya Afya ya Mtoto wa Madrasa Mratibu wa Zanzibar Madrasa
Resouce Centre Mwalim Hassan Abdi Bakar amesema Jumuiya hiyo hutayarisha siku
hiyo kwa ajili ya kuwapatiwa watoto wa madrasa huduma za Uchunguzi wa afya zao
sambamba na watoto waliopo majumbani.
Amesema
Jumuiya hiyo kwa kushirikiana na wafazili wao wakiwemo Aga khan na Jonson and
Jonson wamekuwa wakitoa huduma mbali mbali kwa watoto ikiwa ni pamoja na huduma
za uchunguzi wa afya.
Hata hivyo
ameiomba jamii kuiunga mkono Jumuiya ya Zanzibar Madrasa Resource Centre kwa
kujitokeza kila wanapohitaji kuwapeleka watoto,sambamba na kufungua madrasa
katika sehemu ambazo hazina madrasa huku akisema Jumuiya ipo tayari
kushirikiana nao.
Madaktari wa
magonjwa mbali mbali kutoka wilaya ya Mkoani walishirikiana na jumuiya hiyo kufanya
uchunguzi wa macho,meno,masikio,masikio na koo pamoja na magonjwa mengine
ikiwemo kupima virusi vya ukimwi kwa watoto na watu wazima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni