Habari

Ijumaa, 4 Oktoba 2013

Makamu wa Kwanza ataka Vijana washirikishwe katika kupanga mikakati ya kitaifa



 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza wakati akifungua mjadala wa vijana kuhusu dawa za kulevya, uliofanyika hoteli ya Bwawani Zanzibar
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na vijana wa “Sober houses’ baada ya kufungua mjadala wa vijana kuhusu dawa za kulevya, uliofanyika hoteli ya Bwawani Zanzibar.
Na Hassan Hamad OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha vijana katika utayarishaji wa mikakati ya kitaifa.
 
Amesema vijana wanaweza kutoa mchango mkubwa wa kimawazo katika utayarishaji wa mikakati na mipango mbali mbali ya kitaifa ikiwemo ya kupambana na dawa za kulevya na UKIMWI.
 
Maalim Seif ametoa rai hiyo katika hoteli ya Bwawani, wakati akifungua mjadala wa vijana juu ya kupambana na dawa za kulevya.
 
Amefahamisha kuwa bado vijana hawajashirikishwa ipasavyo katika mikakati hiyo, na kuwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao wanashiriki katika mjadala huo kulizingatia kwa umakini suala hilo, ili kuweza kufanikisha mipango ya serikali.
 
Akizungumzia mikakati ya kupambana na dawa za kulevya amesema ni pamoja na kudhibiti uingizwaji wa dawa hizo pamoja na  kutoa elimu kwa vijana ili kuelewa athari za matumizi ya dawa hizo ambazo zimekuwa zikiwaathiri zaidi vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.
Amesema tayari serikali imeanzisha kampeni maalum ya kutoa elimu maskulini kuhusiana na athari za dawa hizo, na kwamba lengo lake ni kuisambaza elimu hiyo katika skuli zote za Unguja na Pemba.
 
Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais amesema ni jambo la kufurahisha kuona jumuiya mbali mbali na mashirika ya watu binafsi zinaonesha mshikamano na kuwa bega kwa bega na Serikali  katika kuwaokoa vijana na wananchi dhidi ya janga la dawa za kulevya.
 
Amesema biashara na matumizi ya dawa za Kulevya limeendelea kuwa tatizo kubwa duniani, tatizo ambalo limekuwa likisababisha  athari mbaya kwa mataifa ikiwemo Zanzibar.
 
Amefahamisha kuwa hali hiyo inatishia usalama na ustawi wa nchi, na kwamba kuna haja ya kuwepo mshikamano wa hali ya juu baina ya Serikali, Viongozi wa Dini, Jumuiya za Kiraia na katika ngazi ya Kimataifa.
 
Amesema dawa hizo zimekuwa zikileta madhara makubwa kwa vijana waliojitumbwikiza kwenye janga hilo, na kuwafanya kupoteza uwezo wa kufanya kazi, kuenea kwa maradhi  ya Ukimwi, sambamba na kupotea kwa fedha nyingi katika kuwatibu na kuwarekebisha kitabia.
 
Ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na taasisi mbali mbali katika kulikabili janga hilo, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa fedha kwa nyumba za kurekebisha tabia “sober houses”.
 
Mapema akizungumza katika mjadala huo, mratibu wa mradi wa JEE NIFANYEJE, unaojishughulisha na maamuzi ya kiafya na kijamii kwa vijana, bi Khadija Riyami amesema matatizo ya vijana yanapaswa kutambuliwa kuwa ni ya jamii nzima.
 
Bi. Khadija ambaye anafanya kazi katika Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika mjini Washington, amesema wakati umefika kuyazungumza matatizo ya vijana bila ya woga, hatua ambayo itawasaidia vijana kujitambua na kufanya maamuzi sahihi katika mizunguko ya kimaisha.
 
Mjadala huo wa siku moja, umeandaliwa na taasisi inayojihusisha na utoaji wa mafunzo ya biashara na habari Afrika Mashariki (EABMTI), kwa kushirikiana na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni