4th October 2013
B-pepe
apa
Katika marekebisho ya Sheria hiyo ya Magazeti, vifungu viwili ambavyo ni 36 na 37, vitafanyiwa marekebisho ambavyo vinataja ongezeko la faini kwa chombo cha habari kutoka Sh. 150,000 ya sasa hadi Sh. 5,000,000.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrais na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema hatua ya serikali kuwasilisha muswada huo inaonyesha nia mbaya ya kutaka kuua uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), alisema muswada huo ambao unatarajia kuwasilishwa katika mkutano wa Bunge utakaoanza mjini Dodoma Oktoba 29, mwaka huu, tayari serikali imeutangaza katika Gazeti la Serikali namba 34 Juzuu ya 94.
Mbali na Sheria ya Magazeti, muswada huo unakwenda kurekebisha Sheria ya Elimu, Sheria Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, Sheria ya Elimu ya Juu ya Bodi ya Mikopo, Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sheria ya Ugaidi na Sheria ya Vyuo Vikuu.
“Muswada huu wa Sheria unakwenda kuirekebisha Sheria ya Magazeti ya 1976 ambayo sasa hivi imezusha mzozo baada ya Waziri kutumia vibaya sheria mbovu na kandamizi na kufungia magazeti ya MWANANCHI, Mtanzania na kuendelea kulifungia gazeti la Mwanahalisi,” alisema.
Mnyika alisema katika hali ya kushangaza, Serikali badala ya kuirekebisha Sheria ya Magazeti kwa kukifuta kifungu cha 25 ambacho kinaifanya sheria hiyo kuwa mbaya na kandamizi, inapeleka bungeni kurekebisha kifungu cha 36 na 37 kwa kuongeza faini kwa vyombo vya habari.
Alifafanua kuwa kifungu cha 35 na 36 vinavyokwenda kurekebishwa, badala ya kwenda kupunguza majanga kwa vyombo vya habari, sasa wanakwenda kuongeza majanga kwa kuamua kuongeza faini kwa vyombo vya habari kwenye vifungu hivyo.
Alisema sheria ilikuwa inasema kwamba adhabu kwa chombo cha habari kinachofanya kosa faini ni Sh. 150,000, lakini sasa inaongezwa kuwa Shilingi milioni tano baada ya kuvifanyia marekebisho vifungu hivyo.
Alisema pamoja na faini hiyo kuongezeka, kifungu cha kufungiwa chombo cha habari kinabaki pale pale.
“Jambo la hatari katika sheria hiyo mbovu imetoa nafasi kwa serikali ambayo yenyewe ndiyo mlalamikaji, yenyewe ndiyo inaendesha mashtaka, yenyewe inachunguza, yenyewe ndiyo inatoa hukumu bila mamlaka nyingi kuthibitisha kama madai hayo ni ya ukweli au ya uongo, lakini wanakutoza faini,” alisema.
Mnyika alisema kimsingi, vifungu hivyo ni majanga kwa vyombo vya habari kwa sababu yapo magazeti na vyombo vingine vya habari ambayo yanaendeshwa kwa shida kutokana na kukosa matangazo kutoka Serikalini na wadau mbalimbali.
Alisema uamuzi huu wa serikali ni wazi kuwa unakwenda kuvinyonga vyombo vya habari kwa kuongeza faini.
Alisema lingekuwa jambo la afya kama serikali ingeweka utaratibu mzuri, badala ya yenyewe kuwa na mamlaka ya kulalamika, kuhukumu na kuchunguza ingeviachia vyombo vingine vifanye kazi hiyo kama vile Baraza la Habari Tanzania (MCT) au Mahakama ili kutenda haki kwa vyombo vya habari.
Mnyika alisema muswada huo unapaswa kutafakariwa kwa makini na wadau wa habari kwani iwapo utapitishwa itakuwa kitanzi kwa vyombo vya habari na uhuru wa vyombo vya habari hautakuwapo sasa.
Alisema muswada huo nyongeza ya kifungo imefanyiwa kwenye eneo linalohusu kanuni ya adhabu (panel code), juu ya marekebisho vifungu vya 55 na 63 vya sheria ilivyokuwa awali.
“Katika kipengele cha kanuni ya adhabu, kuna kipengele kimeongezwa kinachohusu hotuba za uchochezi na za chuki. Kinachotia shaka katika kipengele hiki ni neno chuki ambalo limetafsiriwa siyo tu kwamba kutoa chuki dhidi ya dini nyingine au ya kijinsia, lakini wameeleza ni pamoja na hotuba zinazohusiana na siasa,” alisema.
Alisema inashangaza muswada huu kuletwa kipindi hiki wakati nchi ipo katika utata juu ya mchakato wa kuandika Katiba mpya, Katiba ambayo imetoa haki za msingi ikiwamo haki za uhuru wa habari, haki za uhuru wa maoni na haki za kupata taarifa.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah, alipoulizwa kuhusu muswada huo, alithibitisha kuwapo na kwamba utapelekwa kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo itauchambua kabla ya kuwasilishwa Bungeni.
“Hatuoni kinachoweza kuuzuia muswada huo kuwasilishwa Bungeni, Kamati ya Bunge itakapouchambua inatoa ushauri na kuwasilishwa Bungeni,” alisema Dk. Kashilillah.
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni