WILAYA YA WETE.
Wakaazi wa kisiwa kidogo cha Kokota Wilaya ya Wete kisiwani Pemba, wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kuwatatulia kero zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.
Wakaazi hao 370, wametoa shukrani hizo mbele ya MakamO wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, alipotembelea kisiwa hicho kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Community Forest Pemba.
Katika risala yao iliyosomwa na mwalimu Juma Ali Hamad, wamesema KUWA kwa kipindi kirefu walikuwa wakilazimika kufuata huduma za maji na elimu katika mji wa Wete AMBAPO KWA SASA wamefarijika baada ya kuja kwa miradi hiyo miaka miwili iliyopita.
Amefahamisha kuwa kwa sasa wanafaidika na huduma ya umeme wa nguvu za jua (solar power) ambapo kila nyumba imewekewa taa moja ya kuonea, maji safi na salama yanayotokana na uvunaji salama wa maji ya mvua, pamoja na kuwepo skuli mpya ya msingi ambayo tayari watoto wameanza kusoma.
Hata hivyo wameiomba serikali na wafadhili kuiendeleza miradi hiyo ili kila nyumba iweze kupata umeme kikamilifu, pamoja na kujenga kituo cha afya pamoja na nyumba za walimu ili kuondosha usumbufu kwa walimu wanaosomesha skuli hiyo ya kisiwa kidogo cha Kokota.
Mradi huo unaosimamiwa na Community Forest Pemba kwa mashirikiano na Community Forest International chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya, pia unajishughulisha na utengenezaji wa majiko sanifu, upandaji miti na ufugaji.
Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amewapongeza washirika hao wa maendeleo kwa kuamua kupeleka huduma hizo katika kisiwa hicho, jambo ambalo pia limeisaidia serikali katika mipango yake ya maendeleo.
Amesema KUWA Serikali itaendelea kushirikiana na wafadhili hao ili kuona miradi hiyo inakuwa endelevu na kuwanufaisha wakaazi hao na taifa kwa ujumla.
NAYE Mwakilishi wa Community Forest International kutoka Canada DAFMEN HARDIE amesifu ushirikiano walioupata katika utekelezaji wa miradi hiyo, na kwamba dunia iMEjifunza suala la mashirikiano kutoka Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni