Kampuni ya Ujenzi wa Bandari ya Jamuhuri ya Watu wa China { CHEC
} imeonyesha shauku ya kutaka kujenga Bandari kubwa hapa Zanzibar kwa lengo la
kuifanya Zanzibar kuwa katika ramani ya Dunia kwa utoaji wa huduma za Kimataifa
za usafiri wa Baharini.
Kauli hiyo imetolewa na Muwakilishi wa Kampuni hiyo yenye Tawi
la Ofisi yake Nchini Tanzania Bwana Xu Xinpei wakati akizungumza na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
Bwana Xu Xinpei alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na eneo zuri
la uwekezaji katika masuala ya usafiri wa Bandari Sambamba na Utalii jambo
ambalo Kampuni hiyo imevutiwa kutaka kuwekeza katika Sekta hizo.
Alisema mradi huo ambao kitaalamu umekisiwa kugharimu zaidi ya
Dola za Kimarekani Milion 40 unaweza kutoa fursa kwa meli kubwa za
Makontena pamoja na Watalii kutoka Bara la Asia kuitumia Bandari hiyo.
Alisema hatua hiyo mbali ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu
uliopo kati ya Jamuhuri ya Watu wa China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla
lakini pia utaongeza kasi ya Kibiashara katika mwambao wa Afrika
Mashariki.
“ Tumekuwa tukishuhudia ongezeko kubwa la uwekezaji ndani
ya Visiwa vya Zanzibar ambalo linaonekana kutawaliza zaidi na wawekezaji wa
Bara la Ulaya wakati uwezo kama huo unawezekana pia kufanywa na wawekezaji wa
Bara la Asia hasa China “. Alisema Mwakilishi wa Kampuni hiyo ya ujenzi wa
Bandari ya China Bwana Xu Xinpei.
Akizungumzia suala la uwekezaji katika Sekta ya Utalii Bwana Xu
Xinpei aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuipatia Kampuni yake
eneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa Hoteli kubwa ya Kitalii hapa Nchini.
Alisema ujenzi wa Hoteli hiyo unaweza kuamsha ari kwa wageni na
watalii kutoka Kisiwa cha Hainan Nchini China kutembelea Zanzibar kitendo
ambacho kitaongeza kasi ya ushirikiano wa pande hizo mbili.
Alieleza kwamba Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa ikivunja
rekodi ya idadi kubwa ya watalii wanaotembea na kuzunguuka maeneo mbali mbali
ya Kihistoria Ulimwenguni.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi aliuomba Uongozi wa Kampuni hiyo kufanya mawasiliano na
Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA } na ile ya Ardhi ili
kuona malengo waliyoyapanga yanafanikiwa na kuleta ustawi wa pande zote
mbili.
Balozi Seif alisema Zanzibar na China na hasa Kisiwa cha Hainan
zimekuwa na uhusiano wa kipindi kirefu kutokana na watu wake pamoja
na mimea inayofanana kimazingira.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
alikutana kwa mazungumzo na Balozi wa Malawi Nchini Tanzania Balozi Flossie
Gomile Tijaonga ofisini kwake Vuga.
Katika mazungumzo yao viongozi hao waligusia uhusiano na
ushirikiano uliopo wa muda mrefu kati ya Tanzania na Malawi ambao umeasisiwa na
Viongozi wa mwanzo wa Mataifa hayo.
Alisema bado upo umuhimu wa kuendelezwa kwa uhusiano huo
kutokana na Historia ya kudai uhuru kutoka kwa wakoloni iliyosimamiwa na
Rais wa Kwanza wa Tanzania Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere na mwenzake wa
Malawi Marehema Kamuzu Banda.
Naye kwa upande wake Balozi wa Malawi Nchini Tanzania Balozi
Flossie Gomile Tijaonga alisema Mataifa hayo mawili yamekuwa yakishirikiana
kiuchumi kwa kipindi kirefu.
Balozi Flossie Gomile alisema Malawi imekuwa ikiitumia Bandari
ya Dar es salaam kwa miaka mingi kupitishia bidhaa na mizigo yake kitendo
ambacho kinastahiki kiendelezaw kwa faina ya pande hizo mbili.
Mwanadiplomasia huyo wa Malawi Nchini Tanzania ameipongeza
Zanzibar na Watu wake kutokana na mazingira mazuri pamoja na ukarimu wa watu
wake unaotoa fursa ya watu wa mataifa mbali mbali duniani kupendelea kutembelea
Zanzibar.
Alisema hiyo inatokana na Historia kubwa ya Zanzibar katika
Nyanja za Kimataifa hasa katika masuala ya Biashara na Utalii.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni