Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe ameipa siku moja Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari (TPA) kutaja majina ya watu wanaoiba mafuta katika bomba kubwa la kupakulia mafuta bandarini (SBM).
Alisema wezi hao bila woga wowote wametoboa bomba hilo ambalo ujenzi wake umeigharimu serikali mamilioni ya fedha, kuunganisha mabomba yao chini kwa chini kisha kunyonya mafuta hadi kwenye vituo vyao vya kuhifadhia mafuta.
“Haiwezekani wizi huo ukafanyika bila TPA kuwajua wahusika kwa sababu hujuma hii inaonyesha kuwa inafanywa na watu wenye utaalamu wa hali ya juu,” alisema Dk Mwakyembe jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam kuhusu changamoto na mafaniko katika utendaji wao wa kazi.
Alisema wezi hao wamekuwa wakiibia serikali lita 35,000 hadi 40,000 za mafuta katika kipindi kisichojulikana. Ujenzi wa bomba hilo ulikamilika takriban mwaka mmoja uliopita.
Alisisitiza, “Wizi umepungua kwa kiasi kikubwa TPA katika hilo nawapongeza, lakini wapo wachache ambao siyo waaminifu wamebuni mbinu mpya za kuihujumu serikali. Nataka mpaka Jumatatu (kesho) saa 6 mchana niwe nimeletewa hayo majina.”
Alisema wizi huo unafanyika katika Kampuni ya kuhifadhia mafuta ya Tipper, huku akiagiza kampuni hiyo kuvunja mkataba na kampuni ya ulinzi inayolinda mafuta hayo.
Alisema kutokana na uzito wa suala hilo anashirikiana na Wizara ya Nishati na Madini ili kuhakikisha kuwa wote waliohusika wanachukuliwa hatua.
“Serikali haitakaa kimya katika hili, kilichofanyika ni hujuma ambayo ingeweza kuangusha uchumi wa nchi na kuzorotesha huduma za kijamii. Ni lazima wahusika washughulikiwe” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk Mwakyembe aliutaka uongozi wa TPA kuachana na mpango wake wa kupeleka boti na mitambo mingine kwenye karakana zilizoko Mombasa, Kenya, kwa ajili ya matengenezo, “Huu mpango ni wa ulaji wa wachache tu.”
Alisema mamlaka hiyo inatakiwa kujipanga kwa kuandaa bajeti itakayowasaidia kujenga karakana yake
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni