Na Is-haka Mohammed,Pemba. Wananchi wa Shehia ya Mgagadu wamesema kuwa wanakabiliwa na tatizo la uhaba wa madarasa na walimu wa sayansi katika skuli yao Mizingini jambo ambalo linachangia kwa watoto wao kutofanya vizuri.
Wakizungumza na Sauti ya Istiqama huko Mgagadu baadhi ya wananchi wamesema kuwa uhaba wa madarasa hayo na ukosefu wa walimu kumekuwa kukirejesha myuma maendeleo ya elimu katika sheria ya Mgagadu.
Juma Makame Juma ni Mmoja kati ya wananchi hao ambaye amesema kuwa Mwalimu wa Sayansi ni mmoja ambaye anasomesha masomo ya baolojia na kemisti,huku pia akisomesha katika skuli ya Ngwachani hivyo kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwaongezea walimu wa Sayansi.
Naye Hafidh Juma amesema kuwa wamejaribu kuanzisha ujenzi wa banda lenye vyumba vinne vya kusomea na kufikia katika hatua ya kuezekwa,ambapo serikali ilisema italimaliza lakini ni mwaka wa tano sasa ahadi hiyo haijatekelezwa.
Sheha wa Shehia ya Mgagadu Bi Mafunda Ramadhani Mtipura amethibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema kuwa Rais Mstaafu na aliyekuwa Waziri wa elimu wa wakati huo Harroun Ali Suleiman waliahidi kulimaliza banda hilo yapata miaka mitatu iliyopita.
Hata hivyo amesema yeye akiwa ni sheha wa shehia hiyo ameshachukua juhudi mbali mbali ya kulipeleka suala hilo wilayani lakini ufumbuzi bado haujapatikana.
Na kaimu Afisa Mzamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Bi Ramla Abass Farhani amesema tatizo la uhaba wa walimu katika skuli hiyo wanalitambua na kulifanyia kazi,lakini amesema talizo hilo lipo nchi nzima na sio Mgagadu pekee, hivyo serikali kupitia Wizara ya elimu wamekuwa wakitafuta njia za kulipatia ufumbuzi.
Aidha amewahimiza wananchi wa kijiji hicho cha Mgagadu na vijiji vyengine kuwahamasisha watoto wao wanaohitimu masomo ya sayansi kusomea ualimu,badala ya kukimbilia kusoma katika fani za udaktari na uhasibu pekee kwani ndiyo njia itakayosaidia kuondosha tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni